Na Mwandishi Wetu
MKAZI wa Lindi, Karume Karume (41) aliyesumbuliwa na uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake kwa zaidi ya miaka 25, leo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kufanikiwa kufanyiwa upasuaji rekebishi na watalaam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuondolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tano.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Rekebishi na Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Rekebishi Dkt. Laurean Rwanyuma aliyeongoza jopo la watalaam wenzake kumfanyia upasuaji uliodumu kwa saa nne, amesema baada ya uchunguzi wa kina kukamilika, iligundulika kuwa Karume ana uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake.

Uvimbe huo ulikuwepo shingoni, begani na kifuani. Ugonjwa huo unaitwa Plexiform Neurofibromatosis ambao matibabu yake ni kuondolewa kwa njia ya upasuaji hivyo Agosti 30 mwaka huu mgonjwa huyo alifanyiwa upasuaji.
Dkt. Rwanyuma amesema, ugonjwa aliopata Karume siyo wa kuambukiza bali ni ugonjwa wa kuzaliwa nao ambao ameurithi kutoka kwa ama mmoja wa wazazi wake au wazazi wake wawili wenye ugonjwa huo ambao hushambulia mishipa ya fahamu na kujitokeza kwa njia mbalimbali.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, amesema mara baada ya kumpokea Karume Agosti mwaka huu, hospitali ilifanya jitihada za dhati kuhakikisha anaonwa na madaktari bingwa kwa kumfanyia vipimo mbalimbali ili kubaini mwenendo wa matibabu yake.
Amewapongeza waandishi wa habari kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Dar Es Salaam (DCPC), kumuibua mgonjwa huyo na kumleta hospitalini hapo kwani ndipo penye madaktari bingwa bobezi wa upasuaji rekebishi walioweza kumpa huduma stahiki na kumrejeshea mwonekano unaompa faraja na tabasamu.

Dkt. Mhaville amewaomba wasamaria wema kuendelea kujitokeza kuchangia huduma kwa watu wasiokuwa na uwezo akiwemo Karume ili kukamilisha malipo ya huduma alizopata kupitia namba ya malipo 994501766575 yenye jina Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa upande wake, mjomba wa Karume Salum Idobelele amesema alianza kuhangaika na Karume akiwa na miaka 16 baada ya kupata uvimbe huo na baadae kubahatika mwaka huu kukutana na waandishi wa habari wa DCPC ambao walibeba jukumu la kumtafutia msaada wa matibabu kwa kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke na kisha kupewa rufaa ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.