Na Lucy Ngowi
DODOMA: MTEGO wa inzi wa matunda ni moja ya teknolojia mpya inayotumika kudhibiti visumbufu vya mimea kwa njia ya kibiolojia bila kutumia viuatilifu vyenye sumu.
Kaimu Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti Visumbufu vya Mimea kwa Njia ya Kibiolojia kilichopo Kibaha, Pwani, David Mwamanda amesema hayo katika maonesho ya Kitaifa yanayoendelea Jijini Dodoma.

Mwamanda amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kupunguza matumizi makubwa ya viuatilifu vyenye sumu kwa kutumia teknolojia rafiki na sahihi ili kulinda afya ya mlaji, afya ya mzalishaji, kutunza mazingira na kuhimili ushindani wa soko la kimataifa.
Amesema kuwa mbinu shirikishi zinazotumika kudhibiti visumbufu kwa njia ya kibaolojia huzalisha mazao ambayo yako huru dhidi ya viuatilifu vyenye sumu, hivyo bidhaa zake huwa za bei ya juu ukilinganisha na mazao yaliyozalishwa kwa kutumia viuatilifu vya sumu.
“Aina mojawapo ya teknolojia hiyo ni mtego wa inzi wa matunda. Teknolojia hiyo inafanya kazi kwa kuvutia mdudu kutokana na rangi ya mtego.

“Ndani ya mtego kuna kichocheo kilichowekwa kwa ajili ya kumvutia inzi dume wa matunda. Inzi dume akiingia ndani ya mtego akifikiria anakutana na inzi jike, lakini kuna aina ya sumu imewekwa, hivyo akiingia anakufa.
“Inzi dume akifa, uzalishaji wa inzi wa matunda unapungua kwa sababu hawakutani na inzi jike. Hivyo, teknolojia hiyo itawezesha matunda kama maembe, machungwa, maboga na mengineyo kukua na kukomaa kwa njia salama na ya uhakika bila kutumia viuatilifu vyenye sumu,” amesema.
Kituo hicho kinasimamia ubora wa viuatilifu hai na wadudu rafiki waliosajiliwa nchini.
Pia kinatoa mafunzo kwa wakulima, wataalam wa ugani na wadau wa kilimo kuhusu udhibiti wa visumbufu kwa njia ya kibiolojia.