Na Danson Kaijage
DODOMA: WANANCHI wametakiwa kutoa kipaumbele katika suala zima la usafi, na kuufanya kuwa sehemu ya maisha yao badala ya kusubiri kupewa amri ya kuufanya.
Ofisa afya wa Jiji la Dodoma, John Lugendo amesema hayo alipozungumza na wananchi wa Kata ya Ipagala Jijini Dodoma kuhusu umuhimu wa kufanya usafi na utunzaji wa mazingira.
Lugendo amesema usafi na utunzaji wa mazingira iwe sehemu ya maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, ni sehemu ya maisha badala ya kusubiri kuanza kusukumana na watendaji wa Serikali.
Amesema iwapo wazazi au walezi watazingatoa kutoa elimu kwa watoto wao juu ya umuhimu wa kufanya usafi na kutunza mazingira ipasavyo hakuna familia ambayo itasukumwa na watendaji wa serikali juu ya kufanya usafi majumbani au mitaani.
“Jamii inatakiwa kutambua wazi kuwa usafi ni maisha na usafi lazima uanzie nyumbani kwako wewe na familia yako bila kuwa na usafi thabiti hakuna afya thabiti na kama hakuna afya thabiti hakuna uchumi imara.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunafanya usafi wa mazingira na usafi wa mwili maana yafaa nini kuonekana umeulamba wakati unakotoka ni pa ovyo na panaweza kukusababishia maradhi ya milipuko,”.
Amewaelekeza watendaji wa mitaa kuhakikisha wanachukuliwa hatua watu wote ambao hawajitokezi kushiriki usafi wa mazingira kwa maelezo kuwa sheria zipo zinazowataka watu wote kufanya usafi na kuhakikisha mazingira yao ni safi na salama.
Kwa baadhi ya washiriki wa usafi katika Kata ya Ipagala wameeleza jinsi wanavyojivunia kufanya usafi katika maeneo yao huku wakisema usafi unaongeza thamani ya maeneo.