Na Danson Kaijage
DODOMA: WAKUU wa Taasisi za Serikali wametakiwa kutoa taarifa zao za utekelezaji wa shughuli za maaendeleo kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hasani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Gerson Msigwa, ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Februari 17, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari Jijini hapa, wakati Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), ulipotoa taarifa yake,
Msigwa ambaye pia ni Msemaji mkuu wa Serikari wakati akimkaribisha Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu (TANROAD) Ephatar Mlavi, amesema ni wajibu wa taasisi hizo kuhakikisha zinatoa mawasilisho ya taarifa ya maendeleo kadri walivyopangiwa.

Naye Mkurugenzi huyo wa TANROAD, Mlavi amesema Serikali imefanikisha kujenga mtandao kwa barabara za lami,madaraja na viwanja vya ndege ambavyo vipo katika hali mzuri.
Amesema Katika kipindi hicho, barabara zenye urefu wa kilometa 15,625.55 zimekuwa katika hatua mabalimbali za utekelezaji ambapo barabara zenye urefu wa kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Aidha, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,052.94 na madaraja mawili zimefanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina na Serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami.
“Vilevile, Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja kumi unaendelea. Aidha, miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami.
“Katika kipindi tajwa madaraja makubwa tisa yamekamilika kujengwa kwa gharama ya Sh.i Bilioni i 381.301 kama ifuatavyo: Gerezani (Dsm), Daraja jipya la Tanzanite (Dsm), Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida). “Amesema Mlavi.
Katika maelezo yake amesema kuwa Madaraja 10 ambayo ni Kigongo Busisi (Magufuli Bridge – Kilometa 3.0), Lower Mpiji (Meta 140), Mbambe (Meta 81), Simiyu (Meta 150), Pangani (Meta 525), Sukuma (Meta 70), Kerema Maziwani (meta 80), Kibakwe (meta 30), Mirumba (Meta 60) na Jangwani (Meta 390) ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya Sh. Bilioni 985.802.
Amesema jumla ya Madaraja makubwa 19 yako kwenye maandalizi ya kujengwa ambayo ni: Godegode (Dodoma), Ugala (Katavi), Kamshango (Kagera), Bujonde (Mbeya), Bulome (Mbeya), Chakwale (Morogoro), Nguyami (Morogoro), Mkundi (Morogoro), Lower Malagarasi (Kigoma), Mtera (Dodoma), Kyabakoba (Kagera), Mjonga (Morogoro), Doma (Morogoro), Sanga (Songwe), Kalebe (Kagera), Ipyana (Mbeya), Mkondoa (Morogoro), Kilambo (Mtwara) na Chemchem (Singida).
Katika kipindi cha miaka hiyo minne hali ya barabara kuu na zile za mikoa imeendelea kuimarika ambapo barabara zilizo katika hali nzuri na wastani zimekuwa karibu asilimia 90 ya jumla ya mtandao wote wa barabara wenye Kilometa 37,225.72.