Na Mwandishi Wetu – MAELEZO Zanzibar
ZANZIBAR: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amewaomba Wakuu wa Mikoa ambao itafanyika mikutano ya Maofisa Habari kuandaa maeneo kwa ajili ya shughuli ya upandaji miti.
Lengo likiwa kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira.

Msigwa amesema hayo leo Aprili 05, 2025, wakati akiongoza maofisa habari wa Serikali kupanda miti 2000 katika msitu wa Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ulioshuhudiwa pia na Mkuu wa Mkoa huo,. Ayoub Mohammed Mahamoud.
Amesema maofisa hao watakuwa sehemu ya upandaji miti hiyo kwa ajili ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza, kuhifadhi mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Sisi kama maofisa habari wa Serikali nchini ni lazima tuwe sehemu ya kutengeneza nchi ya kijani na hilo litawezekana kwa kushiriki katika zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini” amesema.

Ameeleza upandaji miti huo utakuwa endelevu ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za kutunza na kuhifadhi mazingira na kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.
Maofisa Habari hao wa Serikali wapo visiwani Zanzibar kushiriki Kikao Kazi cha 20 cha siku nne kilichoanza Aprili tatu, 2025 ambacho kinatarajiwa kuhitimishwa Aprili sita, 2025.