Na Mwandishi Wetu
ANTANANARIVO, MADAGASCAR: BOHARI Kuu ya Dawa ya Tanzania (MSD) imefanya ziara rasmi katika Bohari Kuu ya Dawa ya Madagascar (SALAMA) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya, hususan katika maeneo ya usambazaji na ununuzi wa pamoja wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Taarifa imesema zara hiyo imeongozwa na Meneja wa Masoko ya Kikanda wa MSD, Nabila Hemed, aliyeambatana na maofisa mbalimbali wa taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakiwa katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo, wajumbe wa MSD walikutana na uongozi wa SALAMA ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Claude Ramanantoanina.
Taarifa imesema Viongozi hao walijadiliana kuhusu njia bora za kushirikiana katika utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa pamoja wa bidhaa za afya kwa nchi za SADC – mpango ambao Tanzania kupitia MSD imekabidhiwa jukumu la kuratibu.
Nabila amewasilisha mada kuhusu uwezo na mafanikio ya MSD katika kuhifadhi, kusambaza na kusimamia ununuzi wa dawa na vifaa tiba, akisisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa SADC, ikiwemo Madagascar, kutumia kikamilifu mpango huo wa pamoja kwa manufaa ya wananchi wake.

Mpango huo unalenga kupunguza gharama za bidhaa za afya, kuongeza upatikanaji wa dawa bora na kuimarisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya katika ukanda wa SADC, hivyo kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa nchi wanachama.
Wawakilishi wa MSD na SALAMA walikubaliana kuendelea kubadilishana taarifa, uzoefu na mbinu bora za kiutendaji katika maeneo ya uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
MSD pia iliualika rasmi uongozi wa SALAMA kutembelea Tanzania kwa ziara ya kujifunza na kuendeleza mazungumzo ya kimkakati.

Mazungumzo hayo yamefanyika Agosti nane, 2025, kando ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi wa SADC unaoendelea jijini Antananarivo.
Waliohudhuria ni Nabila kutoka MSD, Mwenyekiti wa Bodi wa SALAMA Claude, Balozi Mindi Kasiga kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania pamoja na Ofisa Sheria Mkuu wa MSD, Ukundi 
