Na Mwandishi Wetu
ARUSHA :: WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB ili kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano endelevu.
Amesema miundombinu hiyo iwe yenye kuleta tija kwa wananchi katika kupata huduma za intaneti kwa bei nafuu, zenye ubora wa juu na kuaminika.
Kauli hiyo ameitoa jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano na TEHAMA “Connect to Connect Summit 2024”.
Amesema wadau wa sekta ya TEHAMA na Mawasiliano wanatakiwa kuiunganisha Afrika kwenye miundombinu ya mawasiliano ili kuchochea ukuaji wa ujenzi wa uchumi wa kidijitali barani Afrika utakaosaidia katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
” Tuendelee kuimarisha ushirikiano wetu uliopo kama wadau wa sekta ili kufanikisha utekelezaji wa mikakati pamoja ya kuunganisha Afrika na kujenga uchumi wa kidijitali kwa nchi zetu…”Amesema Silaa.
Katika kuhakikisha Afrika inaungwa kwenye miundombinu ya mawasiliano, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirila la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Cecil Francis kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo amesema kuwa Shirika limefanikiwa kuunga nchi zabalbali za Afrika.
Amesema tayari Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ( SADC) zimeungwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuwezesha nchi wanachama kukuza matumizi ya TEHAMA na kurahisisha shughuli za maendeleo.
“Hivi sasa tunaendelea na juhudi za kuunganisha nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma hadi katika jimbo la Kalemie,” amesema hatua hiyo itasaidia kukuza ushiriakiano na Kikanda katika kuchochea ukuaji wa maendeleo.
Katika kuuganisha Tanzania .Cecil amesema kuwa Shirika limeendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano pamoja na kuunganisha zaidi ya Wilaya 100 kati ya 139 katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuchochea kasi ya ujenzi wa Tanzania ya Kidigitali.
TTCL imedhamini huduma ya intaneti kwenye Mkutano huo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Shirika katika kutoa huduma ya Intaneti kwenye Mikutano ya Kimataifa na Kitaifa, ambayo imekuwa chachu ya kuwezesha washiriki kuendelea kufanya shughuli zao kidigitali.
Mkutano wa Connect to Connect 2024 unafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Septemba 18-19 2024 ambapo unakutanisha wadau mbalimbali kutoka zaidi ya nchi 20 kwa ajili ya kujadili kwa kina ukuaji wa sekta ya TEHAMA na Mawasiliano na umuhimu wa kuunganisha Afrika kwenye miundombinu ya mawasiliano.