Na Lucy Ngowi
PWANI: CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania ( TUGHE), kimetimiza miaka 30 toka kilipoanzishwa na mafanikio lukuki.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Hery Mkunda amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania.
Mkunda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vyama vya Wafanyakazi Afrika Mashariki na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Duniani, ameyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kutengeneza kanzidata ya kutambua idadi ya wanachama wao.
“Tumeweza kujua mwanachama gani yupo wapi, kila mwezi tunaweza kujua nani amechangia kiasi gani, lakini tunaweza kujua nani ameingia, nani ametoka kwa mwezi,” amesema.
Mafanikio mengine ni kuwaingiza wanachama takribani 15,000 kutokana na malengo waliojiwekea.
“Pia tumeboresha utendaji kazi wetu. Kama chama tuna mpango kazi tunaufanyia kazi, tumeweza kuutekeleza kwa zaidi ya asilimia 90. Haya kwetu ni mafanikio,” amesema.
Awali amesema jukumu lao kubwa ni kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wafanyakazi na mwajiri ili kuweka mazingira rafiki sehemu za kazi.
“Chama cha wafanyakazi kinafanya kazi kama daraja kuwaunganisha mwajiri na wafanyakazi ili mwajiri apate haki yake na atimize malengo yake ambayo yeye mwenyewe hawezi kuyafanya bila kushirikiana na wafanyakazi.
“Lakini pia na wafanyakazi waweze kupata mkate wao kwa nguvu ambazo wanakuwa wamemuuzia mwajiri,” amesema.
Amesema katika kufanikisha hili, chama jukumu lake ni kutoa elimu inayoonyesha mahusiano kati yao na mwajiri, ikiwa ni pamoja na kutimiza majukumu yao.