Na Mwandishi Wetu
KIGOMA: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema Tanzania inahitaji mabadiliko ya kweli na uongozi wenye mawazo mapya ili kuokoa uchumi wa taifa ambao, kwa maoni yake, umeharibiwa.
Akihutubia wakazi wa Nguruka, Kigoma Kusini, Mwalim amesema licha ya nchi kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali, maendeleo yamekuwa ya kusuasua, hasa katika mikoa kama Kigoma.

“Miaka 64 tangu tupate uhuru ndiyo Kigoma mnaiona lami kwa mara ya kwanza, katika nchi hii iliyojaa madini na ardhi ya kutosha kwa kilimo cha kila aina,” amesema.
Mwalim ametoa mfano wa Kenya, akieleza kuwa mafanikio ya uchumi wa nchi hiyo yanatokana na kuthamini elimu na kutumia rasilimali kwa tija.

Akijibu hoja ya umri katika uongozi, Mwalim amewataka vijana kutokukatishwa tamaa kwa hoja hiyo, akimtoa mfano wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Urais siyo suala la umri. Mwalimu Nyerere aliongoza taifa hili akiwa kijana na ndiye alikuwa rais mwenye umri mdogo kuliko wote waliowahi kuliongoza taifa hili,” amesisitiza.
Amewataka wananchi, hususan vijana, kumpa nafasi ili kuonyesha namna ambavyo kizazi kipya kinaweza kuleta mageuzi.
“Chagueni CHAUMMA. Huu ndiyo wakati wa kujipima na kuamua tunaipeleka wapi nchi yetu. Nipimeni kwa dhamira yangu, siyo maneno tu, maana kizazi cha sasa si kizazi cha zamani,” alisema.