Na Danson Kaijage
WIDON Matayo, aliyekuwa diwani wa Kata ya Iseke, Manyoni, amedai kunyanyaswa na kudhalilishwa na baadhi ya wagombea wenzake ndani ya CCM wakati wa mchakato wa kura za maoni.
Matayo amewataja Dkt. Pius Chaya, mgombea ubunge wa Manyoni, na Joshua Nzwile, mgombea udiwani kata ya Iseke, kuwa walimkebehi kwa misingi ya ulemavu, wakisisitiza kuwa “kata hiyo haiwezi kuongozwa na mlemavu”, kwa kuwa ni sehemu alikozaliwa Dkt. Chaya.
“Walinidhalilisha waziwazi, wakisema ulemavu wangu ni mkosi kwa kata hiyo,” amesema Matayo, akieleza kuwa alikosa haki sawa ya kushiriki mchakato wa uchaguzi wa ndani.
Katika hatua nyingine, usiku wa kuamkia Agosti tatu, 2025 Enock Lisasi, mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Wilaya ya Manyoni kutoka tawi la Isimbangulu, alikamatwa nyumbani kwa Nzwile akiwa na orodha ya majina ya wajumbe wapatao 200 na Shilingi 90,000, sehemu ya zaidi ya milioni 15 alizodaiwa kutumia kuhonga wajumbe kwa niaba ya Dkt. Chaya na Nzwile.
Matayo anadai kuwa Lisasi alipobanwa alikiri kutumwa na wagombea hao wawili. Tukio hilo lilithibitishwa na msimamizi wa kura za maoni kata ya Iseke, Barnaba Mushi, ambaye alisema Lisasi alikabidhiwa kwa polisi wa kituo cha Manyoni.
Hata hivyo, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambqna ba Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Singida, Sosthenes Kibwengo, amesema hana taarifa za kukamatwa kwa Lisasi kwa kuwa yupo nje ya mkoa huo kwa sasa.
Alipotafutwa, Dkt. Chaya amejibu kwa ufupi kwamba malalamiko hayo yapo katika mchakato wa chama, hivyo hawezi kuyazungumzia kwa sasa.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Manyoni, Maimuna Likunguni, amethibitisha kupokea malalamiko na kusema yanashughulikiwa ndani ya vikao halali vya chama.