Na Lucy Ngowi
DODOMA: SERIKALI imeshauriwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya barabara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza ajali zinazotokana na ubovu wa barabara nchini.
Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Itigi, John Msita, alipokuwa akichangia makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.
Msita amesema maendeleo ya uchumi wa kati wa juu hayawezi kufikiwa bila uwepo wa mtandao imara wa barabara zinazopitika wakati wote, akisisitiza kuwa miundombinu hiyo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya Taifa.
Ameeleza kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zimeharibu kwa kiasi kikubwa barabara nyingi za lami zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), hali inayochangia ongezeko la ajali za barabarani, hususan za mabasi, zinazosababisha vifo na majeruhi.
“Tunashuhudia mafuriko yakiharibu barabara na kusababisha ajali kutokana na mashimo na uharibifu wa miundombinu. Ni muhimu Serikali ichukue hatua za haraka kufanya ukarabati ili barabara ziweze kupitika wakati wote,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa barabara katika uchumi, Msita ameitaja barabara ya Mkiwa–Itigi–Mitundu–Rungwa hadi Makongorosi (Chunya) kuwa kiungo muhimu kinachounganisha mikoa ya Songwe, Mbeya, Tabora, Singida na Dodoma, pamoja na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi jirani za Zambia na Malawi.
Amesema kuchelewa kukamilika kwa barabara hiyo kunakwamisha jitihada za kukuza uchumi na kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu, akisisitiza kuwa barabara bora ni msingi wa ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika hoja nyingine, Mbunge huyo ameeleza kuwa sehemu kubwa ya mtandao wa barabara nchini unasimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), ambapo nyingi ni za udongo na huathirika zaidi wakati wa mvua.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wabunge kushinikiza kuongezwa kwa bajeti ya TARURA ili kuboresha barabara hizo na kuhakikisha zinapitika kwa urahisi mwaka mzima.
Aidha, Msita amezungumzia changamoto za matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Manyoni, akibainisha kuwa uwepo wa mapori ya akiba ya Rungwa, Muhesi na Kizigo unazuia wananchi kupanua shughuli za kiuchumi licha ya uwepo wa rasilimali nyingi.
Amependekeza Serikali ipitie mipaka ya mapori hayo kwa kuyapunguza ili kutoa nafasi kwa wananchi kufanya kilimo na ufugaji, akieleza kuwa ongezeko la watu limeongeza mahitaji ya ardhi.
Pia amegusia changamoto za upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa na vyeti vya kuzaliwa, akisema wananchi wengi vijijini hukumbana na matatizo ya mtandao wanapofuatilia huduma hizo.
Ameitaka Serikali kuboresha mifumo ya utoaji huduma hizo ili kupunguza usumbufu kwa wananchi na kuimarisha uwazi katika upatikanaji wake.

