Na Lucy Ngowi
MOROGORO: MTAFITI wa mazao jamii ya mikunde kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Mussa Tamba ameshauri wakulima na wananchi kutumia mazao ya mikunde katika lishe kwa kuwa yana kiwango kikubwa cha protini.
Tamba ambaye ametoka Kituo cha TARI Ilonga kilichopo Kilosa Morogoro amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Habari hii, katika Maonesho ya kilimo ya nanenane mwaka huu 2025, Kanda ya Mashariki yanayoendelea mkoani Morogoro.

Ametaja mazao hayo kuwa ni mbaazi, kunde, dengu, njugu mawe, choroko, na soya.
Ameeleza kuwa zao la soya lina asilimia 37 hadi 40 ya protini na mafuta karibu asilimia 22. Pia lina madini ya chuma na zinko kwa wingi, ambayo ni muhimu kwa afya ya binadamu.
Amesema Katika maonesho ya kilimo yanayoendelea, TARI Ilonga imewasilisha teknolojia ya mbegu bora na elimu juu ya kanuni bora za kilimo cha mikunde ili kuongeza tija kwa mkulima.

“Kwa upande wa mbaazi, kuna aina saba zilizogawanywa katika makundi matatu kulingana na muda wa kukomaa.
“Muda mfupi wa miezi minne, mbegu aina ya Komboa haitegemei msimu na inaweza kupandwa wakati wowote ikiwa kuna chanzo cha maji.
“Muda wa kati ya miezi sita, Tumia mbegu aina ya Ilonga 14 M1 na Ilonga 14 M2 , hupandwa msimu wa masika nchini nzima lakini si zaidi ya mita 1900 kutoka usawa wa bahari.

“Muda mrefu wa miezi tisa mbegu aina ya Karatu, Kiboko na Mali. hazifai kupandwa mikoa ya Pwani kutokana na hali ya hewa,” amesema.
Amesema mazao mengine kama chorizo, kunde na soya pia yana aina mbalimbali zinazopendekezwa kulingana na maeneo na misimu ya mvua.
Akielezea Choroko ametaja aina nne kuwa ni Nuru, Imara, TARIGRAM 1, TARIGRAM 2, hukomaa kwa siku 65 hadi 70 na hustawi vizuri hadi mita 1500 kutoka usawa wa bahari.
Pia Kunde ambazo zimegawanyika katika makundi mawili, zisizotambaa ni Vuli 1, Vuli 2 ambazo hukomaa kwa siku 65-70.
Zinatambaa ni Fahari, Raha 1, Raha 2, Tumaini, Vuli AR 1 na Vuli AR 2 ambazo hukomaa kwa miezi mitatu na hupendekezwa kupandwa masika. Vuli AR 1 na 2 zina uwezo wa kukinzana na magugu na wadudu wa gugu chawi.
Amesema soya zipo aina nne
Ambazo ni Uyole Soya 1 hadi 4 , Uyole Soya 2 inapendekezwa zaidi ukanda wa mashariki, hususan msimu wa masika. Zao hili linahitaji unyevu wa kutosha.
Amehimiza wakulima kufuata kanuni bora za kilimo kama kupanda kwa nafasi sahihi, matumizi ya dawa za kuzuia na kutibu magonjwa ya mimea, na kuchagua aina bora za mbegu kulingana na eneo.