Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni amesema wanategemea kupokea vitendea kazi mbalimbali vitakavyosaidia kutatua changamoto ya utendaji kazi.
Masauni amesema hayo wakati wa ziara yake katika Mkoa wa Dodoma alipokuwa akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa kabla ya kuzindua miradi na kuzungumza na wananchi kwenye Mkutano wa hadhara wilayani hapo.
Ametaja vitendea kazi vitakavyopokelewa kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa ni magari ya kuzima moto, helikopta, na boti.
Pia amesema wizara yake itafanyia kazi na kuziondoa changamoto zote za Vyombo vya Usalama vilivyo chini yake alizozibaini kwenye ziara hiyo.
Katika ziara hiyo Waziri Masauni amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Dodoma ikiwemo uzinduzi wa vituo vya Polisi, Shule ya Sekondari na maabara ya shule ya Sekondari.
Amekiri watendaji wa Vyombo vya Usalama vilivyo chini ya Wizara yake kufanya kazi kwa ufanisi na kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha amani na usalama inakuwepo wakati wote.