Na Danson Kaijage
DODOMA: SAMWEL Malecela ameshinda kura za maoni za Ubunge kupitia CCM katika Jimbo la Dodoma Mjini, huku Anthony Mavunde akiibuka kidedea Jimbo la Mtumba, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa uchaguzi Irimina Mushonge.
Katika Dodoma Mjini, Malecela alipata kura 2,804 sawa na asilimia 43 kati ya wagombea nane. Wapinzani wake waliokuwa karibu ni Samwel Kisaro (23%) na Paschal Kinyele (10%). Jumla ya kura halali zilikuwa 6,226 kati ya 6,288 zilizopigwa.
Kwa upande wa Mtumba, Mavunde alipata ushindi mkubwa kwa kura 2,082 sawa na asilimia 80.9 kati ya wagombea wanne, akifuatiwa na Mussa Luhamo aliyepata asilimia 12. Kura halali zilikuwa 7,352 kati ya 7,446 zilizopigwa.
Hata hivyo, baadhi ya wagombea wa Dodoma Mjini hawakusaini makubaliano ya matokeo wakidai kuwepo kwa malalamiko, ambayo msimamizi amesema yatashughulikiwa kwa njia ya maandishi rasmi.