Na Lucy Lyatuu
MKUU wa Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), Naibu Kamishna Mstaafu Wa Polisi Dkt Lazaro Mambosasa amewataka makamanda wa polisi kuacha kurudi nyumbani na vyeo vya Ukamanda kwani inaweza kuleta taswira ya hofu bali wawe ni watu wa kawaida wenye kujichanganya na raia
Aidha amesema licha ya kustaafu, ameongezwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuendelea kuongoza chuo cha DPA.Ameahidi kufanya kazi kwa tija zaidi ya mara mbili hadi tatu kwa kipindi alichoongezewa katika utumishi wake.
Dkt Mambosasa amesema hayo Dar es Salaam katika hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na Chuo hicho kilichopo barabara ya Kilwa.
Ametoa asante kwa wote waliohusika kuandaa sherehe za mwisho wa utumishi wake kwa umma na kwamba alichotendewa sio rahisi kuamini .
“Nilijua ni kundi dogo linalojumuika kuniaga, niliwaasa hata viongozi mwanzoni kuwa wasiwashirikishe wanafunzi kwa ajili ya kuchanga ili kuniaga kwa kuwa wana majukumu yao binafsi, lakini nimeshangaa leo kuona kundi kubwa likishangilia,” amesema Dkt Mambosasa na kuongeza kuwa hiyo ni kutokana na walioguswa kwa matendo aliyowatendea.
Ameshukuru kwa zawadi ya gari aliyopewa na chuo hicho kwani imemfikirisha sana hadi akakumbuka akiwa mkuu wa Chuo alitafuta magari kwa ajili ya chuo na alifanikiwa kupata matatu lakini hakuchukua hata moja lakini leo (jana) ameweza kuzawadiwa gari.
“Hata nilipokuwa Kanda Maalum nilifanya mipango mingi kuhakikisha magari yanapatikanika lakini muda wangu ulipokwisha niliondoka na kuyaacha, hivyo asanteni sana,” amesema.
Amesema kwa vijana waliopo chuoni hapo kwa ajili ya masomo wazingatie zaidi masomo ya moduli zote, wahakikishe wanapimana kwenye mitihani ili watokapo wawe imara kama ambavyo Mkuu wa Majeshi nchini amekuwa akisisitiza.
Amesema hatokubali DPA kusiwe na viwango vya kimataifa na kwamba mapenzi yake kwa chuo hicho yatakoma iwapo wanafunzi hawatozingatia mafunzo.
“Kote nilikopita nimeacha alama, someni kwa bidi ili mtakapokuwa na nyota ziwe ni zenye utendaji uliotakiwa,” amesema na kuongeza kuwa kwa mkataba alioongezwa anataka DPA yenye nidhamu na viwango.
Kuhusu mafanikioya uongozi wake na familia amewataka makamanda kuwa watu wa kawaida maana wapo wanaokwenda na ukamanda hadi kanisani na uraiani.
Amesema ili ukubalike ni vyema kujichanganya na watu wote kuwa na nidhamu huku ukitambua nafasi yako ni kutekeleza majukumu kwa kuzingatia weledi.
“Kuongezwa muda wa kazi hakuji hivihivi, ninaendelea kufanya kazi kwa uaminifu na kwamba katika suala la kusherehekea kustaafu tufanye hivi pia kwa askari wadogo ili kuongeza kuthaminiana na kuishi kwa Pamoja,” amesema.
Akimwakilishi Mkuu wa Majeshi Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi na Mkuu wa Utawala na Mipango Dk Isaya Hasanali amesema Dkt Mambosasa ameonesha mfano wamabadiliko chanya katika maeneo yote alikopita kiutumishi na kwmaba hajafanya vibaya ndio maana ameongezwa muda.
“Hongera kwa nidhamu ya kazi, imesababisha ustaafu kwa heshima, nidhamu mbovu haiwezi kumfikisha yoyote pae alipofika Mambosasa<” amesema na kuongeza kuwa wapo askari waliostaafu zaidi ya 3000 lakini walioongezwa mkataba hawafikii 1000.
Amesema hiyo ni kutokana na bidi nakwamba sio jambo la ajabu akaonesha bidhii zaidi kwa kipindi hicho na wengine waaige mfano wake.