Na Mwandishi wetu
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka Viongozi wa Dini nchini kote kutumia majukwaa yao kusaidia Serikali kutoa elimu sahihi kuepuka na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ya Mpox, Kipindupindu na Marbug.
Akimwakilisha Waziri wa Afya Jenister Mhagama, kwenye Mkutano wa Viongozi wa dini kuhusu tahadhari ya magonjwa ya mlipuko na Bima ya Afya kwa Wote, Dkt. Mollel ameeleza hayo.
Dkt Mollel amesema viongozi wa dini wana wajibu kiroho kuhakikisha wanailinda jamii na maradhi yanayoepukika kwa kutumia majukwaa yao ya ibada.

“Tunazungumza nanyi kwa niaba ya waumini, viongozi wa dini kote nchini isaidieni Serikali kutoa elimu sahihi ya kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama Mpox, Kipindupindu na Marbug,” amesema.
Amesema serikali imeendeleza jitihada za afua mtambuka ili kuhakikisha nchi inabaki salama.
“Wakati tukifuatilia wasilisho tumeona ramani ya Tanzania ikiwa nyeupe lakini wenzetu wanao tuzunguka wameshapata visa vya baadhi ya magonjwa ya mlipuko, sasa niwaombe muemde mkazungumze na wanajamii ili ramani ya Tanzania izidi kubaki nyeupe,” amesema.
Naye katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema ipo haja ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili wananchi ambao ni waumini kwenye nyumba za ibada kuwa salama na kuendelea na majukumu yao.
“Tumekubaliana tunatoka hapa tukiwa na nia moja, tunaenda kuwahimiza waumini wetu lakini pia na sisi wenyewe kwa usafi ndio kila kitu, baadhi ya mila na desturi zetu zinazokuwa hatarishi tuziepuke na sisi tuwajibike na kuhakikisha tunaendelea kuwa salama na mwisho wa siku nchi yetu kwa ujumla itakuwa salama,” amesema.
Kwa upande wao wawakilishi wa viongozi wa dini wameipongeza Serikali kwa kutumia majukwaa ya dini kuendelea kufikisha elimu ya afya kwa umma na kuahidi kwenda kuwahimiza waumini dhidi ya magonjwa hatarishi ya mlipuko.