Shoo awataka wadau wajifunze teknolojia mpya
Na Lucy Ngowi
GEITA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo anatarajiwa kufungua Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo Bombambili, Manispaa ya Geita.
Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Samwel Shoo amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari jana, na kuongeza kuwa Tume ya Madini inashiriki maonesho hayo kwa mwaka wa nane mfululizo, imeandaa huduma mbalimbali za elimu kwa wadau wote wa sekta ya madini.

Amesema maonesho hayo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wachimbaji, wachenjuaji, wafanyabiashara na wadau wengine kubadilishana ujuzi na mbinu bora za kazi.
Pia amesema ni fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya madini na sekta nyingine za kijamii na kiuchumi.
“Ni wakati wa wadau wa madini kujifunza teknolojia za kisasa zinazohusu utafiti, uchimbaji na uchenjuaji. Wachimbaji wa viwango vyote, wawekezaji pamoja na wananchi wenye nia ya kuwekeza wanapaswa kufika kujipatia maarifa sahihi,” amesema Shoo.

Ameongeza kuwa banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake, ikiwemo Tume ya Madini, litatoa elimu ya kina kuhusu mnyororo mzima wa shughuli za madini.
Amehimiza Watanzania kulitumia ipasavyo banda hilo kwa ajili ya kupata taarifa muhimu zinazoweza kuwasaidia katika kufanya maamuzi ya uwekezaji.
Maonesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu: ‘Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025′.