Na Lucy Ngowi
MBEYA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameonesha kufurahishwa na juhudi za Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kuwawezesha vijana wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia elimu ya ufundi stadi itakayowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Majaliwa ameonyesha furaha hiyo alipotembelea banda la VETA katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Vijana Yanayoendelea mkoani Mbeya, ambapo alishuhudia vijana wenye ulemavu wakionyesha umahiri wao katika ushonaji wa nguo na teknolojia ya kompyuta.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Balozi wa VETA katika Kitengo cha Watu Wenye Mahitaji Maalum, Francis Anthony, ambaye ni fundi na sasa mwalimu wa kompyuta, amesema alihitimu mafunzo ya kitaalamu kupitia VETA na kwa sasa anawafundisha wengine.
“Nilianza kama mwanafunzi, sasa ninafundisha. Huu ni uthibitisho kuwa VETA imewajengea uwezo vijana wenye mahitaji maalum,” amesema Anthony.
Naye Riziki Ndumba, mwanafunzi kutoka VETA Songea anayesomea ushonaji, amesema alianza bila ujuzi wowote lakini kupitia msaada wa walimu na viongozi wa chuo, amehitimu kozi ya miaka miwili kwa mafanikio.
“Nataka kuwa mfano kwamba hata sisi wenye ulemavu tunaweza kufanya kazi na kujitegemea,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano kwa Umma kutoka VETA Makao Makuu, Elmer Sarao, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika kuwafikia vijana wote, wakiwemo wenye ulemavu.
Amesema mmoja wa walimu waliopo sasa ni mhitimu mwenye ulemavu aliyesoma VETA kuanzia mwaka wa kwanza hadi wa tatu, na sasa anafundisha katika chuo cha mafunzo Morogoro.
“Huyu ni mfano hai kuwa ulemavu si kikwazo cha ufanisi. Tunajivunia kuwalea na kuwaendeleza vijana hawa,” amesema Sarao.
Kwa mujibu wa VETA, uwepo wa vijana wenye mahitaji maalum katika vyuo vyao ni sehemu ya mkakati wa serikali kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kujenga taifa lenye nguvu kazi jumuishi, mahiri na yenye tija.