Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka za mikoa, halmashauri na taasisi za elimu nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la mwaka 2023, kwa ufanisi kulingana na majukumu yao.
Aidha Majaliwa amezitaka halmashauri ziweke kipaumbele katika kuanzisha na kuendesha shule za amali ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri na hatimaye kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Ametoa maelekezo hayo leo Ijumaa Februari 14, 2025 wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 18 wa Bunge la 12, bungeni jijini Dodoma.

“Sera na Mitaala hiyo ni maono na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kufanya elimu inayotolewa hapa nchini iwiane na mahitaji ya sasa, lakini pia wahitimu wapate stadi na maarifa yatakayomudu mabadiliko na kasi ya ukuaji wa teknolojia,” amesema.
Pia amesema hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuimarika ambapo katika msimu wa 2023/2024 uzalishaji wa mazao ya chakula ulifikia tani milioni 22.8.
“Kwa kuzingatia uzalishaji huo na mahitaji ya chakula ya tani milioni 17.7 kwa mwaka 2024/2025, nchi itakuwa na utoshelevu wa asilimia 128.
“Hadi kufikia Januari 31, 2025 Wakala imehifadhi jumla ya tani 776,000 za nafaka katika ghala za Wakala zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini,” amesema.
Kwa upande mwingine ametoa wito
kwa wananchi wanaoishi kwenye baadhi ya maeneo nchini yanayopata mvua chache kuchukua tahadhari mapema na kuzalisha mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.
“Hatua hii iende sambamba na kutumia vizuri mavuno yaliyopatikana kwa kutunza chakula cha kutosha katika ngazi ya kaya,” amesema.
Bunge limeahirishwa hadi siku ya Jumanne Aprili nane, 2025.