Mwandishi Wetu
ARUSHA: TAASISI ya Waandishi wa habari ya kusaidia jamii za asili (MAIPAC),imeanza kutoa makoti ya usalama kwa ajili ya kutambuliwa wanahabari wakiwa kazini.

Makoti hayo yanatolewa kwa waandishi ambao ni wanachama wa MAIPAC ili kuwasaidia kufanyakazi katika mazingira salama kuelekea uchaguzi mkuu.
Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC,Mussa Juma akizungumza wakati wa kugawa makoti hayo kwa waandishi wanachama waliopo Serengeti katika Taasisi dada ya MAIPAC ya __Serengeti Media_ amesema lengo la kutolewa makoti hayo ni kuwezesha wanahabari kufanyakazi katika mazingira salama.
Juma amesema, makoti hayo yametengenezwa na Mtandao wa watetezi wa haki za Binaadamu Tanzania(THRDC) na kutolewa kwa Taasisi ya MAIPAC ambayo ni mwanachama wa THRDC.
“THRDC kwa kushirikiana na MAIPAC tunapenda waandishi wa habari wakati wote kufanyakazi katika mazingira salama na makoti hayo wakivaa watawatambulisha hasa pale zinapotokea vurugu”amesema
Amesema MAIPAC pia kwa kushirikiana na THRDC itaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi na usalama kwa wanahabari na sheria na kanuni za Uchaguzi, kuelekea chaguzi mkuu.
Mmoja wa waandishi wa taasisi ya _Serengeti Media_ iliyopo Serengeti mkoa wa Mara Agness Boma akizungumza baada ya kukabidhiwa makoti alishukuru MAIPAC na THRDC kutambua umuhimu wa usalama kwa wanahabari.
Boma amesema watatumia makoti hayo kufanyakazi kwa weledi bila kupendelea chama chochote katika uchaguzi mkuu ujao.
Wakati huo huo, Juma amewataka waandishi wanachama wa MAIPAC kujisajili katika bodi ya Ithibati ili kutambuliwa kisheria na kufanyakazi kisheria za uandishi wa habari.