Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: JOPO la madaktari bingwa wa mifupa, ganzi na wauguzi kutoka Ireland limewasili nchini na kuanza kambi maalum ya siku nne ya matibabu ya mifupa kwa watoto katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Kambi hiyo, inayoendeshwa kwa ushirikiano na madaktari wa MOI, inalenga kuwahudumia watoto wenye miguu iliyopinda, miguu mifupi, matege na mivunjiko ya mifupa.

Akizungumza wakati wa kuwapokea madaktari hao, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema ushirikiano huo na hospitali ya Children’s Health Ireland ya Dublin umeendelea kwa zaidi ya miaka minne, na umechangia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
“Tunashirikiana nao kutoa matibabu ya kibingwa kwa watoto wenye matatizo ya mifupa na pia kujengeana uwezo katika huduma za kibobezi,” amesema Dkt. Mpoki.
Ameongeza kuwa MOI inapanga kuanzisha huduma ya tiba mtandao ili kuwawezesha wagonjwa kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa bila kusafiri umbali mrefu.
Kwa upande wake, Dkt. Paula Kelly, bingwa wa mifupa kwa watoto kutoka Ireland, amesema kambi hizo zimekuwa zikisaidia kubadilishana uzoefu na teknolojia za kisasa katika matibabu ya mifupa.
Naye Dkt. Bryson Mcharo, Mkuu wa Kitengo cha Matibabu ya Mifupa kwa Watoto MOI, amesema wagonjwa wote wanapimwa na wale wanaohitaji matibabu zaidi watafanyiwa upasuaji kwa kutumia kifaa maalum cha kisasa cha Taylor Spatial Frame (TSF) kinachotumika kunyoosha miguu na kurekebisha urefu wa mifupa.
