Na Mwandishi Wetu
MFUMO wa ya sheria za uwekezaji nchini ukiboreshwa utasaidia kuweka mazingira mazuri, yenye uhakika yatakayovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufani Beatrice Korosso amesema hayo
katika kikao cha Kamisheni ya Tume hiyo kilichokaa kujadili rasimu ya taarifa ya sheria zinazosimamia uwekezaji nchini ikiwemo sheria ya Uwekezaj, mkoani Morogoro.
Amesema maboresho hayo yakifanyika yatasaidia kuondoa vikwazo kama urasimu, kodi zisizovutia au taratibu ngumu za kupata vibali vya biashara.

Pia yatasaidia kuongeza ushindani wa nchi katika soko la kimataifa la uwekezaji.
Jaji Korosso amesema maboresho hayo ni muhimu kwa kuwa yataiwezesha nchi kuendana na viwango vya kimataifa vya biashara, uwekezaji na kufanya sheria zake ziwe sambamba na mikataba ya kikanda na kimataifa ili kupata masoko mapya yatakayovutia uwekezaji wa kigeni.
Vilevile maboresho hayo yatachochea uanzishaji wa viwanda, ukuzaji wa ajira, na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo zitokanazo na uwekezaji hivyo nchi itakuwa imejenga mazingira yenye tija ya kiuchumi ambayo yatachangia ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo endelevu.
“Marekebisho ya sheria yanaweza kusaidia kuhakikisha kuwa wawekezaji wa ndani, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati, wanapata fursa sawa za kushiriki katika uchumi.
“Kwa kuweka motisha kwa uwekezaji wa ndani, nchi inaweza kukuza uchumi wa wananchi wake na kupunguza utegemezi wa uwekezaji wa kigeni pekee,” amesema.
Katika hilo amesema tume imepiga hatua kubwa katika kukamilisha taarifa yenye mapendekezo ya maboresho mfumo wa ya sheria za uwekezaji nchini kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, George Mandepo awali alieleza kwamba mapendekezo yaliyotolewa yatasaidia katika kuendana na mabadiliko ya kiuchumi, teknolojia, na utandawazi kama vile teknolojia ya habari (TEHAMA), nishati mbadala, na biashara za mtandaoni zinazohitaji sheria ambazo zinaweza kuruhusu na kuwezesha uwekezaji katika maeneo mapya yanayokua kwa kasi.
Akizungumzia kuhusu uhifadhi wa mazingira na rasilimali asili, Mandepo ameeleza kwamba maboresho ya sheria za uwekezaji ni muhimu katika kuhakikisha kuwa shughuli za uwekezaji zinaendana na ulinzi wa mazingira na kuweka misingi ya kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo ya kiuchumi haiathiri mazingira au kuharibu rasilimali za asili, kama vile ardhi, maji, na misitu.
Amesema maboresho ya mfumo wa sheria za uwekezaji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, usalama wa kisheria katika wawekezaji na uimarishaji wa mifumo ya kiutawala na kijamii.
Pia amesema maboresho ya mfumo huo yanatachochea ukuaji wa uchumi, ajira na kuhakikisha uwekezaji endelevu kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.