Mwandishi Wetu
WANAFUNZI 40 walioteuliwa kuwa Mabalozi wa Uhifadhi na Utalii wilayani Babati, mkoa wa Manyara, wameahidi kuulinda ushoroba wa wanyamapori wa Kwakuchinja uliopo katika Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge, inayounganisha hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara.

Wanafunzi hao kutoka shule nne za sekondari katika eneo la Burunge WMA walitoa ahadi hiyo baada ya kurejea katika ziara ya mafunzo ya uhifadhi na utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, iliyogharamiwa na Taasisi ya Chem Chem Association.
Kiongozi wa wanafunzi hao, Prosper Frank wa Shule ya Sekondari Mbughwe, alisema wamepata maarifa muhimu yatakayowawezesha kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda ushoroba huo.
Amesema kauli mbiu yao ni “Kwakuchinja Corridor Shall Never Die” na wakaomba serikali iwashirikishe katika mikutano ya kutoa elimu ya uhifadhi na utalii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Babati, Ofisa Tarafa Emmiliana Fred ameishukuru Chem Chem kwa kufanikisha mafunzo hayo na kuahidi ushirikiano wa serikali katika kukuza uhifadhi na utalii.
Amesema elimu waliyoipata wanafunzi itawasaidia kuwa mabalozi wa utalii na hata kujiajiri baadaye.
Mkurugenzi wa Chem Chem Association, Clever Zulu, amesema mafunzo hayo yataleta mabadiliko chanya katika uhifadhi na utalii kuanzia Burunge WMA hadi taifa zima. Aliongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali na jamii katika kuendeleza uhifadhi, pamoja na kusaidia sekta za elimu, afya, maji na uwezeshaji wa vijana na wanawake.
Kwa niaba ya wazazi, Dk Benson Andrea aliipongeza Chem Chem kwa uwekezaji wake katika uhifadhi na kuahidi ushirikiano wa jamii zinazozunguka Burunge WMA.





