Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: OFISA Mfawidhi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mkoa wa Dar es Salaam, Yohana Massawe, amewataka waajiri kote nchini kufuata taratibu za kisheria wakati wa upunguzaji wa wafanyakazi ili kuepuka migogoro ya kikazi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Massawe amesema CMA imekuwa ikipokea malalamiko mengi yanayohusiana na upunguzwaji wa wafanyakazi, ambapo changamoto kubwa inajitokeza katika kutokufuata utaratibu unaoelekezwa na sheria.
“Mwajiri anaweza kuwa na sababu halali za kupunguza wafanyakazi, lakini akishindwa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria, hatua hiyo huonekana ni batili,” amesema..
Amebainisha kuwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2023, kifungu cha 39, kinamtaka mwajiri anayetaka kupunguza wafanyakazi kutoa taarifa rasmi na muhimu kwa wafanyakazi wake, kisha kuandaa vikao vya majadiliano ili kujadili namna bora ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Kwa mujibu wa Massawe, majadiliano hayo yanaweza kusababisha makubaliano mbadala kama vile kupunguza mishahara (bila kushuka chini ya kima cha chini cha serikali), kubadilisha vitengo vya kazi, au kupanga upya muundo wa taasisi, badala ya kuachisha wafanyakazi moja kwa moja.
“Lengo la majadiliano ni kufikia mwafaka unaotekelezeka kwa pande zote. Makubaliano hayo lazima yawe kwa maandishi na yahusishe chama cha wafanyakazi au wafanyakazi wenyewe endapo hakuna chama,” amesema.
Massawe ameeleza sababu kuu za upunguzaji ni changamoto za kiuchumi, kiteknolojia au mabadiliko ya kimuundo ndani ya taasisi, amesema mabadiliko hayo yanaweza kusababisha kupungua kwa mahitaji ya nguvu kazi, kwa mfano pale teknolojia mpya inapochukua nafasi ya kazi za watu.
Hata hivyo, alionya kuwa waajiri wengi hushindwa kuzingatia vigezo vya msingi vya upunguzaji na hivyo kujikuta wakikabiliwa na mashauri mbele ya tume.
“Mara nyingi ushahidi unaonyesha sababu ya msingi ipo, lakini kosa linakuwa ni kwenye utaratibu. Ni muhimu waajiri wakajielimisha kuhusu sheria hizi na kuzisoma mara kwa mara,” amesema.
Kwa mujibu wa CMA, mashauri ya upunguzaji kazi yanapaswa kushughulikiwa ndani ya siku 30 katika hatua ya usuluhishi, kabla ya kuhamia hatua ya uamuzi wa upatanishi endapo hakutakuwa na mwafaka.
Massawe amehitimisha kwa kuwataka waajiri kutumia nafasi yao kuhakikisha migogoro ya kikazi inapungua, kwa kuwa kufuata sheria na majadiliano ya wazi ni njia bora ya kulinda haki za pande zote.

