Na Danson Kaijage
DODOMA: WAANDISHI wa habari kupitia vyombo mbalimbali wametakiwa kuandika habari kwa usahihi hususani katika kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025 ili kuondoa migongano ya kisiasa isiyokuwa ya lazima.
Aidha wamekumbushwa utumiaji mzuri wa lugha ya kiswahili kwa nia ya kuikuza, ambayo kwa sasa imekuwa ikitumiwa na mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, utamaduni na Michezo, Khamisi Mwijuma amesema hayo, wakati wa kufunga mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini uliofanyika Jijini Dodoma.

“Kwa sasa kuna jambo muhimu la kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kuwachagua madiwani,Ubunge na Rais, hivyo ni vema kuandika habari kwa usahihi ” amesema.
Kwa kuwa ni mwaka wa uchaguzi. ni vyema waandishi wakafanya kazi kwa weledi mkubwa, kutumia kiswahili sanifu badala ya kuibananga lugha hiyo ambayo inaweza kupoteza maana.
Amesema kada ya uandishi ni muhimu kwa kutoa elimu kwa ujumla wake na kuhakikisha habari zinazoandikwa, zinaandikwa kwa faida ya jamii na siyo vinginevyo.
Pia amewataka waandishi nchini kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni zilizopo kwa nia ya kuwezeaha kuandika habari zenye uhakika zaidi na kuaminika.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni mdau mkubwa wa habari hivyo anatarajia kuona wanataaluma hiyo wakifanya kazi yao. Kwa uhuru lakini wakiwa wanazingatia sheria,kanuni na maadili ya kazi.