Na Lucy Ngowi
GEITA: MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ametoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa ya kushirikiana na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ili kuhakikisha mradi mkubwa wa makazi ya biashara unaoendelea mkoani Geita unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Ametoa wito huo alipofanya ziara katika maonesho ya nane ya teknolojia ya madini yanayofanyika kwenye viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, Geita,
Akiwa katika banda la TBA, Kingalame amesifu ubunifu wa TBA kwa kuanzisha mradi huo ambao unalenga kuboresha hali ya makazi kwa wananchi na watumishi wa umma.
“Ni wazo bora sana ambalo linatafsiri kwa vitendo maono ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora. Tunahitaji sekta binafsi kujitokeza kushirikiana na TBA ili tufanikishe kwa pamoja,” amesema Kingalame.
Ameongeza kuwa mradi huo ukikamilika utaleta manufaa makubwa kwa jamii kwa kuwa utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi na watumishi wa serikali.
“Makazi haya yataleta raha na utulivu kwa wananchi na watumishi. Hii ndiyo tafsiri halisi ya dhamira ya Rais Samia ya kuona wananchi wake wanaishi katika mazingira mazuri na ya kisasa,” amesema.