Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amesisitiza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kutoa elimu yenye viwango vinavyoweza kushindana kimataifa.
Kauli hiyo alitoa wakati wa ziara yake katika chuo hicho mkoani Dar es Salaam, akibainisha kuwa elimu inapaswa kutatua changamoto za mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla.
Katambi amesema CBE inatakiwa kuimarisha tafiti za tija zitakazochochea maendeleo ya elimu, kubaini changamoto zilizopo na kutoa suluhu zinazofaa.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia tafiti za kina katika kutoa ushauri kwa serikali ili kufanya maamuzi sahihi.
Aidha, amehimiza chuo kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, akibainisha kuwa kundi hili lina mzunguko mkubwa wa fedha lakini halijapewa kipaumbele cha kutosha.
Pia amesema CBE inaweza kushirikiana na taasisi za kifedha, hususan benki zinazotoza riba kubwa, ili kusaidia maendeleo ya wajasiriamali.
Katambi pia amegusia umuhimu wa kutambua na kuwarasimisha watu wenye ujuzi walioupata nje ya elimu rasmi, hatua itakayochangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa CBE, Prof. Edda Lwoga, amesema chuo kimeanza kujiendeleza kimataifa kupitia ujenzi wa uwezo wa wahadhiri na kuanzisha programu mpya.
Ofisa Miliki wa chuo, Osward Mtei, ameeleza kuwa ujenzi wa jengo la Metrology umeanza Mei 25, 2023, ukitarajiwa kukamilika Mei 23, 2026, kwa gharama ya jumla ya Sh. Bilioni 26.47.

