Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amelitaka Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kufanya tathmini ya kina ili kubaini njia bora za kufufua viwanda vilivyokufa na kutoa ushauri wa kitaalamu utakaoviwezesha kurejea katika uzalishaji.
Katambi ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake katika shirika hilo, akisisitiza umuhimu wa kuondoa changamoto zinazosababisha viwanda kusimama licha ya kuwepo miundombinu.
Amesema kero kubwa kwa wananchi ni kushuhudia viwanda vilivyopo lakini havifanyi kazi, hali inayokwamisha utoaji wa ajira na kupunguza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Katambi, utafiti ni nguzo muhimu ya maendeleo, kwani huwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazosaidia kupanga na kutekeleza mikakati ya maendeleo kwa ufanisi.
Katambi ameeleza kuwa matokeo chanya ya tafiti huchochea ukuaji wa viwanda, uwekezaji katika sekta ya uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, tafiti husaidia kufahamu mienendo ya kiuchumi katika dunia ya sasa inayoendeshwa kwa kiasi kikubwa na maarifa pamoja na teknolojia.

Ameongeza kuwa Serikali inalitegemea TIRDO kutoa ushauri unaozingatia misingi ya sayansi na teknolojia ili kukuza viwanda imara vinavyoweza kushindana sokoni.
Ushauri huo unapaswa kuzingatia thamani ya fedha, uwekezaji wa viwanda, miundombinu na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Pia amesisitiza kuimarisha teknolojia, ubunifu na uvumbuzi kama vipaumbele vya kukuza ajira na maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi (DED), Ramsons Mwilangali, amesema shirika linaendelea kusaidia sekta ya viwanda kwa kufanya tafiti za teknolojia stahiki, kusimamia na kusambaza matokeo ya tafiti kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.

