Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, ametoa wito kwa wananchi na taasisi husika kuchukua hatua madhubuti kudhibiti mianya isiyo rasmi inayoruhusu uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi viwango nchini.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Katambi amehimiza Watanzania kutumia huduma za TBS ili kuhakikisha bidhaa wanazozalisha au kutumia zina ubora unaokubalika.
Aidha, amewatahadharisha wafanyabiashara wanaokwepa kodi au kuingiza bidhaa duni, akisema vitendo hivyo huisababishia serikali hasara na kuhatarisha afya za wananchi.
Katambi amesisitiza umuhimu wa kupambana na magendo na kuwataka wananchi kujenga tabia ya kukagua viambato vya bidhaa wanazotumia, hususan bidhaa za chakula na vipodozi.
Amesema TBS iko tayari kupokea sampuli za bidhaa na kuzifanyia tathmini ili kuthibitisha ubora wake kabla ya kuingia sokoni.
Ameongeza kuwa changamoto katika sekta ya chakula mara nyingi husababishwa na kutokuzingatiwa kwa masharti ya utunzaji wa bidhaa, akisisitiza kuwa TBS haipaswi kulaumiwa pale ambapo masharti hayo yanakiukwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema viwango vya kitaifa hutengenezwa kwa ushirikishwaji wa wadau na shirika hilo lina maabara nane zinazotambulika kimataifa.
Ameongeza kuwa TBS inaendelea kupanua wigo wa huduma zake kupitia ofisi za kanda na vituo katika bandari na viwanja vya ndege ili kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia nchini.

