Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na Baraza la Ushindani (FCT) kuhakikisha ushindani wa haki katika biashara, hususan kuondoa ukiritimba na kupandishwa kwa bei za bidhaa na huduma.
Akizungumza katika ziara yake Baraza la Ushindani, Katambi amesema ushindani wa haki ni msingi wa ukuaji wa biashara, huku akibainisha kuwa biashara zinapaswa kulinda maslahi ya walaji, kuhakikisha bidhaa zenye ubora, na kufuata sheria kwa haki.
Ameongeza kuwa maboresho ya mgawanyo wa kazi kati ya Tume ya Ushindani na Baraza yamepunguza mzigo na kuongeza ufanisi, huku utulivu ukiwa umeimarishwa katika mazingira ya biashara.

Katambi amesisitiza Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa sera rafiki na maboresho ya kisheria, huku utatuzi wa migogoro ukipewa kipaumbele ili kulinda heshima, muda na maslahi ya wawekezaji.
Aidha, amesema usimamizi wa sheria za ushindani unalenga kumlinda mlaji na kuhakikisha ubora wa huduma, huku utatuzi wa migogoro kwa wataalamu wabobezi ukiimarisha imani katika sekta ya biashara.
Kwa niaba ya Jaji Rose Ibrahim, Dkt. Onesmo Kyauke amesema Baraza la Ushindani lina nafasi ya kipekee kuhakikisha sera za ushindani zinatekelezwa, kuvutia uwekezaji na kulinda maslahi ya walaji.
Ameongeza kuwa Tanzania iko katika kipindi cha ukuaji wa biashara na viwanda, huku Baraza likijipanga kuwa la kisasa na lenye weledi wa hali ya juu kushughulikia changamoto za soko kwa haki na haraka.


