Na Mwandishi Wetu
KIGOMA: MKUU wa Wilaya ya Kasulu, Isaac Mwakisu, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru pamoja na Uchaguzi Mkuu ujao, kwa kuwa matukio hayo ni ya kitaifa, yanaakisi mshikamano wa Watanzania.
Mwakisu amesema hayo leo Jumamosi Septemba Sita, mwaka 2025, wakati wa bonanza la michezo mbalimbali lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiganamo.

Amesema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbizwa wilayani humo kwa siku mbili, Septemba 17 hadi 18, 2025.
Amesema mwenge huo utapokelewa katika eneo la Mvugwe, Kasulu Vijijini, kabla ya kuingia Kasulu Mjini siku inayofuata.
“Maudhui makuu ya bonanza hili ni kuwakumbusha wananchi kuwa Mwenge utakimbizwa katika wilaya yetu.

“Ni muhimu tushiriki kwa wingi ili kuonesha mshikamano wetu na kuthamini amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema Mwakisu.
Pia amesema Mwenge ni alama adhimu ya taifa, na mapokezi yake ni kielelezo cha uzalendo na dhamira ya kudumisha amani, umoja na maendeleo ya taifa.

Amewakumbusha wananchi kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba 29, 2025.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu kwa kusikiliza sera za wagombea na kuwachagua viongozi wanaowakilisha matarajio yao.

Katika mahojiano na Mwandishi wa Habari hii, mmoja wa wananchi Nelstella Kihoza, amesema umati mkubwa ulioshiriki bonanza hilo ni ishara ya mwamko wa kisiasa na uzalendo miongoni mwa wananchi wa Kasulu.
Amesema ni imani pia wananchi watajitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu na Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Naye Mwalimu Yusufu Hamisi amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa ubunifu wa kuandaa bonanza hilo, akisema limewapa ari mpya ya kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu matukio hayo muhimu ya kitaifa.