Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Vijana Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga anahamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma waweze kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika keshokutwa Novemba 27, 2024.
Akiwa katika Kata ya Matiri wilayani Mbinga kwenye fainali za mpira wa miguu mashindano ya Mkuu Super Cup, Kapinga amehamasisha makundi mbalimbali ya wananchi kushiriki katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa utakaofanyika nchi nzima.
” Ndugu zangu, wote tunafahamu kazi kubwa iliyopo mbele yetu ya kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi makini watakaokuwa wasimamizi wa shughuli za maendeleo katika maeneo yetu, kama ambavyo mmejitokeza kwa wingi katika fainali hii, nguvu hii pia tuielekeze keshokutwa Novemba 27,2024, siku ya kupiga kura.” Amesisitiza Kapinga
Kapinga ameendelea kuwakumbusha wananchi kuchagua Viongozi imara, makini na wenye uchungu na maendeleo katika maeneo yao huku akiweka mkazo kuwa viongozi hao wanatokana na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kuhusu fainali ya Mkuu Super Cup ilihusisha timu ya Bodaboda FC na Afya FC ambapo Bodaboda FC iliibugiza timu ya Afya kwa goli tatu, huku Afya ikiambulia goli moja.
Timu zilizoshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika michuano hiyo zimepata zawadi ikiwa ni njia ya kutoa motisha kwa vijana kujihusisha na michezo.