Na Lucy Ngowi
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara unazalisha fursa kubwa za ajira, hasa kwa vijana.
Aidha amesema Serikali inathamini ujasiriamali wa wazawa na inahakikisha wanapata nafasi za kuendeleza biashara zao, jambo linalochangia kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha uchumi wa ndani.
Waziri Kapinga alieleza hayo Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari katika Mkutano ulioandaliwa na Idara ya Habari – Maelezo.

Kapinga alieleza fursa zilizopo katika kilimo biashara, viwanda vya kuongeza thamani ya rasilimali, biashara ya kikanda kupitia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), viwanda vinavyoanzishwa katika kongani, teknolojia na utafiti, biashara mtandaoni, na usambazaji katika minyororo ya thamani.
“Sekta ya viwanda haiwezi kujengwa bila vijana. Serikali imejenga miundombinu, kufungua masoko, kurahisisha mikopo na usajili wa biashara. Sasa ni jukumu la vijana kuchukua hatua,” alisema.
Akizungumzia Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, Waziri Kapinga alibainisha viwanda imara, biashara yenye ushindani na sekta binafsi yenye nguvu kama nguzo za uchumi shirikishi.

Aidha, maboresho ya sera na sheria yameboresha mazingira ya biashara, kuongeza mauzo ya nje ya bidhaa na huduma, na kukuza uzalishaji wa ndani wa bidhaa kama saruji, mabati, flat glass na tiles, huku nchi ikipata ziada ya bidhaa kwa ajili ya kuuza nje.
Vilevile alizungumzia usajili na utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao umeboresha urahisi wa biashara, na kuunganisha mifumo ya taasisi 29 za Serikali na binafsi.
Alisema Maboresho hayo yameongeza idadi ya kampuni na biashara zilizosajiliwa, leseni za biashara na viwanda, na kuongeza kasi ya urasimishaji wa biashara.
Waziri Kapinga pia alieleza miradi mikubwa inayozalisha ajira kwa vijana, ikiwemo Mradi wa Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda Engaruka, Mradi wa Chuma Maganga Matitu na Mradi wa Makaa ya Mawe Katewaka,
Pamoja na uwekezaji wa kongani za viwanda kama Kwala na Modern Industrial Park. Miradi hiyo nazalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa vijana wenye ujuzi wa ufundi, uhandisi, biashara na usambazaji.
Aidha, teknolojia na ubunifu vinatumika kuendeleza viwanda vidogo, kutoa mashine na teknolojia za kuchakata mazao, uzalishaji wa mkaa mbadala, biogas na bidhaa za mifugo.
Waziri huyo alisema, Serikali pia inatoa mikopo nafuu kupitia mfuko wa NEDF, TADB na Mfuko wa Dhamana, ili kuwasaidia vijana kuanzisha viwanda vidogo, biashara za uzalishaji na ubunifu wa teknolojia.
Waziri alisisitiza: “Biashara mtandao na masoko ya kidijitali ni fursa kubwa kwa vijana. Serikali itaendelea kuweka miundombinu, mafunzo na rasilimali ili waweze kufanikisha ndoto zao, kuhakikisha malipo salama, masoko makubwa na msaada wa kitaaluma.”

