Na Lucy Ngowi
KANISA la Watakatifu wa Siku za Mwisho limekabidhi jengo lenye thamani ya sh milioni 595 la kuhudumia watoto lililopo Kituo cha Afya Kimara kwa Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam.
Akikabidhi jengo hilo lililopo ghorofa ya pili katika Kituo hicho, Rais wa kanisa hilo, Juventinous Rubona amesema msaada huo wa ujenzi ni zaka zinazotolewa na waumini wa kanisa hilo
Rubona amesema ujenzi wa ghorofa hiyo ya watoto ulianza mwaka jana kwa kuanza na ngazi zilizogharimu sh milioni 115, kisha ghorofa hiyo iliyogharimu sh milioni 480.
“Mafanikio haya yanatokana na serikali kutoa uhuru wa kuabudu ikiwa ni pamoja na kuruhusu kutoa huduma hii ya kijamii,” amesema.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dk Felister Kimolo amesema,” Ni furaha kubwa kupokea mradi huu uliogharimu kiasi kikubwa cha fedha. Ulianza mwaka jana sasa umekamilika,”.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Malamla Chaulenzi amesema zaidi ya wananchi 100,000 wa Kata ya Saranga wanatibiwa katika kituo hicho.
Amesema kati ya wananchi 450 hadi 600 wanahudumiwa kwa siku, kati ya wanawake 15 mpaka 25 wanajifungua kwa siku, na kila wiki wanapeleka rufaa nne za watoto katika hospitali ya Mloganzila, ndipo wakaona waandike andiko la kuomba jengo hilo kwa ajili ya kuhudumia watoto wadogo hasa wachanga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Kamati ya kusimamia kituo hicho, Thomas Mbogo amelishukuru kanisa hilo kwa msaada huo kwa jamii.