Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam imekagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha zinazotolewa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa Ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Bass Mtemvu amempongeza Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila, na viongozi wote walio chini yake kwa kazi nzuri wanayoifanya hususani utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye masilahi mapana kwa umma pamoja na ushirikiano mkubwa walionao kati ya Chama na Serikali.
Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Mei saba, 2025 Chalamila amesema miradi yote katika Mkoa huo, itakamilika kwa wakati kwa viwango na kuzingatia thamani ya fedha.
Pia amesema mkakati wa Mkoa kwa sasa ni kujenga ghorofa katika majengo ya umma ikiwemo shule, vituo vya Afya kutokana na ufinyu wa watu na ongezeko la watu.
Katika ziara hiyo kanati imekagua ujenzi wa Jengo la Ghorofa la Shule ya Sekondari Mangaya linalojengwa Mbagala, Mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Temeke unaojengwa Chamazi na Kituo cha Polisi cha Kisasa kinachojengwa Toangoma.