Ridhiwani Kikwete Aguswa Na Ajira Pamoja Na Uhakika Wa Soko La Chai Kwa Wakulima
Na Mwandishi Wetu
TANGA: UWEKEZAJI uliofanywa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Wafanyakazi wa Umma (PSSSF), katika Kiwanda cha Chai Mponde, kilichopo Bumbuli Lushoto Tanga, umewezesha ajira kwa wananchi.
Hilo limedhihirika wakati Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ilipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kuona shughuli zinazofanywa na kamati hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema miongoni mwa faida za kiwanda hicho ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi pamoja na uhakika wa soko la chai kwa wakulima.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa uwekezaji kwenye kiwanda hico cha Chai Mponde.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea kiwanda hicho na wajumbe wa kamati kwa lengo la kuona namna kiwanda hicho kinavyofanya kazi.

Pia amepongeza mifuko ya WCF na PSSSF kwa uwekezaji wenye tija wanaoufanya kwenye kiwanda hicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa WCF, Dkt. John Mduma amesema kiwanda hicho kitawawezesha wananchi wa Lushoto, Bumbuli Korogwe na maeneo jirani kupata kipato kitakachowainua kiuchumi kwa kuwa wengi wanategemea zao hilo.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo, Mwanyemi Mdoe ameishukuru serikali kwa hatua iliyoichukua ya kufufua kiwanda hicho, ambacho kinasaidia kukuza Uchumi wao.