Na Lucy Ngowi
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema mfumo wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) ni suluhisho la kisasa linalolenga kuongeza ufanisi, ubunifu na kupunguza gharama za utoaji huduma kwa wananchi kupitia miradi ya kimkakati ya maendeleo.
Hayo yamebainika wakati wa maonesho ya 49 ya Kibiashara yanayomalizika leo mkoani Dar es Salaam, katika banda la PPPC lililopo kwenye maonesho hayo.
Kafulila amesema mfumo huo wa PPP unaruhusu mwekezaji binafsi kushirikiana na taasisi za serikali iwe wizara, idara, serikali za mitaa au mashirika ya umma kwa mkataba wa muda mrefu.
Amesema kupitia mkataba huo, mwekezaji binafsi anajenga miundombinu mipya au kuboresha iliyopo kwa gharama zake, huku akiendesha huduma kwa niaba ya serikali kwa kipindi kilichokubaliwa kabla miundombinu hiyo haijarejeshwa serikalini.
“Lengo la PPP ni kutumia nguvu ya sekta binafsi iwe kifedha, kitaalamu, kiteknolojia au ubunifu kuboresha utoaji huduma kwa umma kwa njia nafuu na endelevu,” amesema.
Amesema mikataba ya PPP hupitia mzunguko wa maisha wa mradi ulioainishwa kisheria, kuanzia kuibua wazo, kufanya upembuzi yakinifu, kupata mbia, kujenga, kuendesha hadi kurejesha serikalini.
Aidha, ameeleza kuwa mkataba bora wa PPP hupimwa kwa vigezo vitatu muhimu vya Sekta binafsi kubeba mianya na hatari kubwa za kifedha na kiutendaji,
Pia gharama nafuu kwa serikali na wananchi, na Manufaa kwa umma kama vile huduma bora, fursa za ajira, na ukuaji wa pato la taifa.
Vile vile amesema katika kuhakikisha uwazi na ushindani wa haki, Sheria ya PPP imeweka njia tatu za kumpata mwekezaji ambazo ni kwa kwa njia ya ushindani wa zabuni,
Pia bila ushindani endapo mradi umetoka kwa sekta binafsi na umekidhi vigezo maalum,
Na kwa utaratibu maalum unaopitia maoni ya Mwanasheria Mkuu na kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri.
Kwa mujibu wa Kafulila, mfumo huo ni jukwaa madhubuti la kuvutia uwekezaji, kupunguza mzigo wa bajeti kwa serikali na kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa manufaa ya Watanzania wote.