Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Bariadi Vijijini, Masanja Kadogosa, ameipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayowanufaisha wakulima, wafugaji na wananchi wa vijijini.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Kadogosa amesema sekta ya kilimo imepiga hatua kubwa kupitia ruzuku za mbolea na pembejeo, pamoja na programu mbalimbali za kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji.
“Ruzuku hizi zimeleta unafuu mkubwa kwa wakulima wetu. Kwa upande wa wafugaji, serikali imeendelea kutoa chanjo za mifugo na kujenga majosho katika maeneo mbalimbali. Katika ilani mpya ya CCM, tumewekewa mpango wa kuongeza maeneo ya malisho kutoka ekari milioni tatu hadi milioni sita ,” amesema Kadogosa.
Mbunge huyo ameongeza kuwa, licha ya mafanikio hayo, bado suala la maji vijijini limepewa kipaumbele maalum.
“Kwa sasa, upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 80.9, lakini bado mahitaji yetu ni makubwa. Tuna mradi mkubwa wa Shilingi Bilioni 440 unaotekelezwa sasa, ambao utapita Busega, Bariadi Mjini, Bariadi Vijijini, Kitilima na Meatu. Mradi huo ukikamilika, tutaondokana kabisa na changamoto ya maji,” amesema.
Kadogosa pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Spika mpya wa Bunge, Mussa Zungu, akisema ana imani ataendesha Bunge lenye ushirikiano na Serikali kwa kuzingatia misingi ya kikatiba.
“Tunatarajia kuwa na bunge lenye mijadala yenye tija kwa wananchi. Spika Zungu ana uzoefu mkubwa, na naamini ataongoza Bunge letu kwa hekima, kuhakikisha bajeti na sheria zinazopitishwa zinaakisi mahitaji halisi ya Watanzania,” amesema.
Kadogosa amesema kuwa mafanikio haya yanaonyesha utekelezaji thabiti wa ilani ya CCM na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma bora na maendeleo endelevu.

