Na Lucy Lyatuu
ASKARI wa Jeshi la Uhifadhi nchini wametakiwa kuyaishi mafunzo waliyopatiwa kwa lengo moja kubwa la kuipeleka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika viwango vya juu kiuhifadhi na kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba alipokuwa akifunga rasmi mafunzo ya Uongozi kwa maofisa 159 na Askari Viongozi 77 katika Chuo cha Pasiansi Fort Ikoma, Serengeti
Wakulyamba amefafanua kuwa kupandishwa vyeo kwa askari hao ni matokeo chanya ya mapenzi makubwa ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la Uhifadhi ili kuliimarisha liweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni na Sheria za nchi kwa maslahi mapana ya Uhifadhi wa Maliasili zilizopo.
“Mafunzo haya ni muhimu sana, hivyo niwahimize kuyazingatia yote mliyofundishwa kwa kipindi chote mlipokuwa hapa chuoni. Mkafanye kazi kwa lengo moja kubwa la kuipeleka TANAPA katika viwango vya juu kiuhifadhi na kiuchumi” Akisisitiza Wakulyamba.
Wakulyamba amewasisitiza wahitimu wote kuepukana na kujihusisha na vitendo visivyofaa kwenye uhifadhi ikiwemo vitendo vya rushwa na matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima wakati wa kutekeleza majukumu yenu ya kila siku.
“Ni jukumu lenu pia kujenga umoja na ushirikiano na askari pamoja na maafisa na kuondoa migawanyiko katika kazi”. Alikazia Wakulyamba
Ameupongeza uongozi wa TANAPA kwa kutoa kipaumbele kwa Wanawake kujipatia mafunzo na upandaji wa vyeo, huku pia amewapongeza askari wote kwa kuhitimu mafunzo haya muhimu, amewapongeza pia wakufunzi kwa juhudi kubwa walizozifanya zilizofanywa na wakufunzi wa mafunzo haya.
“Natumaini mafunzo haya yamewaongezea maarifa, ufanisi na uwezo wa usimamizi wa rasilimali za Wanyamapori na Misitu ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa”. Wakulyamba aliongezea
Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Maendeleo ya Biashara TANAPA Massana Mwishawa amefafanua kuwa Mafunzo hayo yaliyofundishwa kwa njia ya nadharia na vitendo yalijumuisha pia matumizi sahihi ya silaha, ulengaji shabaha, usomaji wa ramani, ujanja wa porini na uongozi wa kijeshi.
Pia wamejifunza maadili ya kijeshi, uraia, ugaidi, ujuzi wa uongozi na kazi za ofisi kwa vitendo, usalama wa mtandao, amri za kudumu za jeshi la uhifadhi, ugavi na usimamizi, ukakamavu, uzalendo na uadilifu.