Nawandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ikiongozwa na Mwenyekiti wake Justine Nyamoga imeelekeza kuanza kutumika kwa miundominu ambayo imekwisha kamilika ili kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Amesema “kumekuwa na wimbi kubwa la miradi ambayo imekamilika lakini haijanza kufanya kazi, hasa katika upande wa vituo vya afya hivyo kamati inaelekeza vianze kutoa huduma haraka”
Nyamoga ameyasema hayo katika kikao cha Majumuisho ya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya afya, elimu na miundombinu inayotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa.
Katika ziara hiyo kamati imetembelea miradi mbalimbali ikiwemo Uboreshaji wa miundombinu ya Hospitali ya Mji Mafinga uliohusisha ujenzi wa jengo la kufulia, jengo la kuhudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum na jengo la wodi ya wazazi.
Mradi mwingine ni wa ujenzi wa barabara za mwamkoa-mbagala yenye uredu wa kilomita 0.50, mdeka-rift valley kilomita 0.37 na bravo kilomita 0.19 na msangarufu kilomita 0.19 kwa kiwango cha lami katika halmashauri ya mji Mafinga.
Pia kamati imeipongeza Halmashauri ya Mufindi kwa kujenga kituo cha afya chenye gharama ya zaidi shs 500,000,000 ambapo chanzo kikuu cha fedha hiyo ni mapato ya ndani ya Halmashauri.
Aidha kamati imeendelea kusisitiziza uwekaji wa taa za barabarani katika miradi yote ya Barabara ya lami ambayo itakuwa ikitekelezwa na Wakala wa Barabara Vijiji na Mijini (TARURA) ili kuboresha usalama na kupendezesha Maeneo husika.
Kwa upande wake Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Zainab Katimba amesema Serikali imeyapokea yote yaliotolewa na kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.