Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUTUBI wa Maktaba Kuu ya Dar es Salaam, Saida Kalokola, amesema kuwa huduma za maktaba zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa, na sasa watumiaji wanaweza kusoma vitabu popote walipo kupitia mfumo wa maktaba mtandaoni, mradi tu wawe wamelipia ada husika.
Akizungumza katika Maonesho ya 32 ya Kitaifa ya Vitabu Tanzania yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Kalokola amesema kuwa awali watumiaji walilazimika kufika maktaba ili kupata taarifa za vitabu, ambapo walipewa kadi maalumu iliyoonyesha mahali kitabu kilipohifadhiwa.
Amesema kwa sasa mchakato umerahisishwa. Ada ya mwaka kwa matumizi ya maktaba mtandaoni ni Sh 10,000, huku ada ya siku ikiwa Sh 1,000. Baada ya kufanya malipo, mtumiaji hutaja kitabu anachokihitaji na anakipata moja kwa moja mtandaoni.
Amesema maktaba inatoa vitabu vya aina mbalimbali, ikiwemo vya masomo, hadithi, pamoja na vitabu vya ziada kwa watoto na watu wazima.
Aidha, amewahimiza wananchi kujiunga na huduma za maktaba, akibainisha kuwa kuna maktaba maalumu kwa watoto kuanzia umri wa miaka miwili na nusu, ambayo ada yake ni Sh 5,000 kwa mwaka, huku wanafunzi wa sekondari wakitozwa Sh 7,000 kwa mwaka.
Pia, ameeleza kuwa kuna huduma za maktaba kwa watu wasioona, zinazotolewa bure, zikiwemo nakala za vitabu vya nukta nundu pamoja na vitabu vya maandishi ya kawaida.

