DAR ES SALAAM: TANZANIA haiwezi kukwepa kutumia bioteknolojia katika kuendeleza sekta mbalimbali za uchumi na huduma kwa jamii.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Cyprian Luhemeja, katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST).
Amesema hiyo ni kutokana na ukweli kuwa, nchi zilizowekeza katika bioteknolojia ya kisasa zimeweza kupata faida kubwa katika sekta mbalimbali za uchumi na huduma kwa jamii.
“Utandawazi unaoendelea duniani umefanikisha maendeleo ya teknolojia mbalimbali na ueneaji wake ulimwenguni kote,” amesema.
Amesema pamoja na kwamba Tanzania haiwezi kukwepa baiteknolojia, kuna baadhi ya wadau ambao wana mashaka au wanapinga matumizi ya teknolojia hiyo hususan katika sekta ya kilimo.
“Hali hii inasababishwa kwa kiasi kikubwa na uelewa mdogo wa dhana ya teknolojia hii hata miongoni mwa wanasiasa, watendaji wa serikali, wataalamu na jamii kwa ujumla,”amesema.
Amesema serikali imeweka mfumo thabiti kuhakikisha kuwa utafiti wa kutumia bioteknolojia ya kisasa unafanyika kwa usalama,
Pia bidhaa zozote zinazotokana na teknolojia zitaruhusiwa kutumika baada ya mamlaka za udhibiti kujiridhisha kuwa bidhaa hizo hazina madhara yeyote kwa afya za binadamu, wanyama na kwa mazingira.
Naye Mwenyekiti wa BST, Profesa Peter Msolla amesema matumizi ya bioteknolojia duniani yameshika kasi kwa kutambua manufaa makubwa yanayopatikana kwenye kilimo, afya, mifugo, viwanda, mazingira, nishati na mifumo mbalimbali zimechangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
0
“Hapa nchini tumeshuhudia ongezeko la bidhaa zitokanazo na bioteknolojia kama viuatilifu, vyakula, mazao na mifugo bora yenye tija kwa mkulima, mbinu za kubadilisha taka za mashambani na viwandani kuwa mbolea na gesi,
“Viuatilifu vya kibiolojia vya kuua viluwiluwi vya mbu, viuatilifu vya kibiolojia kwa ajili ya kuua wadudu waharibifu wanaoshambulia mimea na mazao shambani, hii ikiwa ni mifano michache tu,”amesema.