Na Lucy Ngowi
GEITA: MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), imezieleza fursa mpya za uwekezaji kwenye sekta ya madini na nyinginezo katika maeneo maalum ya kanda hiyo.
Ofisa Uwekezaji Mkuu Kanda ya Ziwa, kutoka TISEZA, Erastus Malai ameelezea fursa hizo katika maonesho ya nane ya sekta ya madini yanayoendelea mkoani Geita, na kuongeza kuwa serikali imejipanga kutoa vivutio vya kipekee kwa wawekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Malai amebainisha kuwa eneo la Buzwagi, lilio Geita, limepangwa kutumika kwa shughuli za uchenjuaji madini.
“Eneo hili lenye ukubwa wa ekari 1333 limeandaliwa kwa miundombinu ya kisasa, ikiwa ni pamoja na majengo, barabara, ofisi, na uwanja wa ndege.
“Mwekezaji anayekuja katika eneo hili hatahitaji kugharamia miundombinu, bali atalenga moja kwa moja kuanzisha kiwanda cha kuchanjua madini,” amesema Malai.

Pia amesema Serikali pia imeandaa maeneo mengine ikiwemo Nala (Dodoma), ekari 607, Kwara (Kibaha, Pwani) ekari 100, na Bagamoyo ekari 151.
Amesema maeneo mengine yaliyoandaliwa kwa ajili ya uwekezaji ni katika sekta za kilimo, uvuvi, utalii, ujenzi wa majengo ya biashara, ufugaji, na utengenezaji wa viwanda.
“Tumeweka mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza dawa, vifaa tiba, uundaji wa magari na boti, bidhaa za ngozi, nguo, na vifaa vya majumbani.
“Buzwagi, ambalo ni moja ya maeneo maarufu kwa shughuli za uchimbaji madini, linatoa fursa ya pekee kwa wawekezaji kutokana na maandalizi ya miundombinu iliyokamilika.

“Hii ni sehemu ambapo wawekeza katika sekta ya madini wanaweza kuanzisha viwanda vya kuchambua na kuchuja madini bila kujali gharama za ujenzi wa miundombinu, kwani tayari zipo,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali pia itatoa vivutio vya kodi kwa wawekezaji watakaoamua kuwekeza katika eneo hilo, pamoja na visivyo vya kodi ili kufanikisha maendeleo endelevu.
Malai ameelezea fursa nyingine katika Kanda ya Ziwa kwamba fursa inatolewa kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
“Sekta ya kilimo, kwa mfano, ina nafasi nyingi za uwekezaji hasa katika mazao ya biashara kama pamba, chai, na kahawa. Uvuvi na utalii pia vinatoa fursa kubwa kutokana na utajiri wa maziwa makubwa na maeneo ya kihistoria.
“Wawekezaji na wafanyabiashara wanahamasishwa kuja kuwekeza kwenye maeneo yetu ya kanda ya ziwa kwa sababu kuna miundombinu inayohitajika kwa shughuli zao,” amesema Malai.
Amesema “Kwa niaba ya serikali, tunatoa wito kwa wawekezaji wote, ndani na nje ya nchi, kuja kuwekeza kwenye maeneo haya muhimu.
“Tutatoa msaada na vivutio vya kodi ili kuhakikisha kwamba uwekezaji unakuwa endelevu na faida kwa pande zote.” Amesema.
Kwa kumalizia, Malai amewahimiza wawekezaji kuja kushiriki katika fursa hiyo mpya, akisisitiza kwamba wakati ni sasa, kwani serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji ni ya kirafiki na yenye tija kwa pande zote.