Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: KAMATI ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Serikali kwa kuanzisha Maabara ya Uidhinishaji wa Vifaa vya Mawasiliano ya Kielektroniki ikiwa ni maabara ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso ametoa pongezi hizo wakati Kamati hiyo ilipotembelea Mradi wa Maabara ya Uidhinishaji wa Vifaa vya Mawasiliano ya Kielektroniki unaotekelezwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Kakoso ameitaka Serikali kuendelea kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya kisekta ili vifaa vya mawasiliano vinavyoingia nchini viwe na viwango vinavyotakiwa kitaifa, kikanda na kimataifa akitolea mfano wa mifumo ya TCRA na TBS kusomana.

Pia TCRA imeshauriwa kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo na umuhimu wa maabara hiyo ili kumwezesha mwananchi kufahamu ubora wa kifaa cha mawasiliano kabla ya kukinunua.
Pamoja na hilo Kamati imesisitiza kwa mamlaka hiyo kuendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza mara kwa mara kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali.
Akitoa taarifa ya maabara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari amesema ujenzi wake ulianza Aprili 2023 na kukamilika Machi, 2024 ikiwa ni mwaka mmoja tu kama ulivyopangwa na inafanya kazi katika maeneo mawili ambayo ni eneo la kupima mawimbi ya redio na eneo ya kupima viwango vya mionzi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi ameishukuru Kamati na kuihakikishia kuwa Wizara imepokea ushauri wote uliotolewa na Kamati kwa ajili ya kuboresha.
Uwepo wa Maabara hiyo nchini kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya 12 Barani Afrika, Nchi nyingine ni Tunisia, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Cameroon, Benini, Togo, Senegal, Mali na Mauritania.