Na Lucy Lyatuu
MAMLAKA ya Serikali Mtandao (eGA) imesema imetengeneza mifumo mbalimbali ya Teknolojia Ya Habari Na Mawasiliano (TEHAMA) inayosaidia kurahisisha kazi za kila siku serikalini.
Aidha imewawezesha wananchi kupata huduma kwa njia ya kidigitali na kwa urahisi zaidi
Meneja Mawasiliano wa eGA, Subira Kaswaga, amesema hayo katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema mamlaka hiyo imepewa jukumu la kisheria kusimamia matumizi ya TEHAMA ndani ya Serikali ili kurahisisha utendaji kazi pamoja na huduma kwa wananchi.
“eGA meendelea kuonesha namna ambavyo Serikali inavyotekeleza mageuzi ya kidigitali kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa wananchi kupitia matumizi ya TEHAMA,” amesema
Amesema miongoni mwa mifumo hiyo ni mfumo wa e-Mrejesho, ambao ni jukwaa la kidigitali linalowawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Serikali kwa njia ya kupeleka maoni, pongezi au malalamiko, huku Serikali nayo ikijibu na kutoa mrejesho wa hatua zilizochukuliwa.
Amesema mfumo huo unapatikana kwa njia tatu, ikiwemo kupitia simu ya mkononi, na unampa uhuru mwananchi kuficha taarifa zake za msingi iwapo hataki kujulikana, huku pia akipatiwa namba ya ufuatiliaji wa taarifa aliyoitoa.
“Kwa mfumo huu, taasisi za umma zinaweza kuona ni malalamiko ya aina gani zinayapokea mara kwa mara, hivyo kumsaidia kiongozi wa taasisi kutambua idara au kitengo kinachosababisha changamoto kwa wananchi, na kuchukua hatua stahiki,” amesema.
Mbali na hilo, mfumo huu pia unasaidia kupima uwajibikaji wa watendaji wa umma kwa kuruhusu ufuatiliaji wa hatua zinazochukuliwa baada ya malalamiko kuwasilishwa. Viongozi wakuu wa Serikali kama Katibu Mkuu Utumishi na Katibu Mkuu Kiongozi wanaweza kuona kwa uwazi taarifa za malalamiko katika taasisi zote za umma.
Kutokana na mafanikio hayo, Subira amesema kuwa mfumo wa e-Mrejesho umeendelea kuipa sifa Tanzania kimataifa, ambapo Julai 7, 2025, eGA ilishinda tuzo ya kimataifa iliyotolewa na Shirika la ITU katika kipengele cha Serikali Mtandao.
“Ni fahari kubwa kwamba mfumo huu umetengenezwa na Watanzania, na leo unatutambulisha kimataifa. Tunawahamasisha wananchi wauitumie mfumo huu ili Serikali iwafikie kwa urahisi na kwa ufanisi,” amesema.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa watumishi wa umma kuhakikisha kuwa maoni na malalamiko yanayowasilishwa kupitia mfumo huo yanashughulikiwa ipasavyo ili kukuza uwajibikaji na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali.