Na Lucy Ngowi
DODOMA:MFUMO wa kidijitali umeanza kutumika katika kupima mahindi ili kuleta tija kwa mkulima.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uhifadhi wa Chakula nchini ( NFRA), Dkt. Andrew Komba amesema hayo katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yaliyoanza Agosti mosi na kufikia kilele chake Agosti nane, mwaka huu.
Amesema mfumo huo wa kidijitali unaonesha namna ambavyo mkulima atapata faida na uhakika wa mazao anayouza NFRA.
“Wakulima wameipokea mizani hii vizuri wakiamini kwamba inawawezesha kupata kiwango sahihi wanachotuuzia na sisi kwetu inatupa kumbukumbu sahihi kwa sababu inaingiza taarifa katika mfumo ambao unatumika katika suala zima la kuhifadhi,” amesema.
Pia amesema ,Wakala huo una jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na usalama wa chakula .
Kwa mujibu wa Dkt.Komba,ili kulitekeleza jukumu hilo NFRA wamekuwa wakinunua na kukusanya chakula na kuhifadhi vizuri kwa utaratibu wa kuhakikisha afya na usalama wa mlaji.
“Ili kuhakikisha chakula kinakuwa salama wakati wote ,tunatumia maghala na vihenge katika kuhifadhi chakula,lakini pia tunawafundisha wakulima kuhifadhi chakula wanacholima katika hali ya usalama badala ya kuhifadhi kizamani.”amesema Dkt.Komba
Maelezo yake ni kwamba, chakula wanachohifadhi kinalenga kuisaidia jamii pale panapotokea uhaba wa chakula na kuwafanya wawe na uhakika wa chakula.