MATUKIO YA UWAJIBIKAJI YALIYOTOKEA KUANZIA JANUARI 2024 HADI DISEMBA 2024
JANUARI 27,2024: Waziri Utalii Zanzibar Simai ajiuzulu
Waziri wa Utalii na Mambo ya kale wa Zanzibar, Simai Mohamed Said amejiuzulu.
Kulingana na picha mjongeo zilizosambazwa na Simai mwenyewe, mwanasiasa huyo alisema kuwa amemwandikia Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi barua hiyo ya kujiuzulu, huku akilalamikia mazingira yasiyo rafiki katika utekelezaj wa majukumu yake ya kila siku.
“Nimefikia uamuzi huu ambao ni mgumu kwa utamaduni kwa Kizanzibari, kutokana na imani yangu kuwa jukumu namba moja la wasaidizi wa Rais, wakiwemo mawaziri ni kumsaidia katika kutekeleza ilani ya chama tawala na ikitokea mazingira yasiyo rafiki katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa ustawi wa wananchi, ni vyema kutafuta jawabu kwa haraka ili kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo iweze kuendelea, na hata ikibidi kukaa pembeni,”.
FEBRUARI 23,2024: Dkt. Biteko afuta likizo za watumishi wote tanesco
Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko ametangaza kufuta likizo kwa watumishi wote wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akiwataka wote wawe kazini kukabiliana na changamoto ya upungufu wa umeme.
Amesema hakuna mtumishi wa Tanesco atatakiwa kwenda likizo wakati huu wa changamoto ya mgawo wa umeme na kwamba, kila mmoja kwenye eneo lake atatakiwa kufanya kazi kwa bidii.
Biteko, ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Februari 23, 2024 wakati alipotembelea chanzo cha kuzalisha umeme cha Kidato mkoani Morogoro.
Hatua hiyo ya Biteko imetokana na kupewa taarifa kwamba, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, kuwa amekwenda likizo.
JUNI 12, 2024: Mkuu wa Mkoa Simiyu atenguliwa
Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenani Kihongosi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akichukua nafasi ya Dk. Yahaya Nawanda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
JUNI 18, 2024: Spika Tulia ampeleka Mpina Kamati ya maadili
Spika wa Bunge Tulia Ackson ameelekeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Akitangaza uamuzi huo bungeni jijini Dodoma leo Jumanne, Juni 18, 2024 Tulia amesema kuwa Mpina amedharau mamlaka ya Spika na Bunge kwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
Itakumbukwa Mpina alipewa wiki moja kuwasilisha ushahidi wake baada ya kulieleza Bunge kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amelidanganya bunge katika sakata la uagizaji wa sukari.
JULAI 6,2024 :Samia: Nimemuondoa Kidata TRA, angedata
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa sababu za kumuondoa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata kwa kusema aliona mwisho wa siku ‘atadata’ (atachanganyikiwa).
Imeandaliwa na Lucy Ngowi