Kwa Miaka 54 Benki Yake Imetoa Dola Za Kimarekani Bilioni Tisa
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: BENKI ya Maendeleo ya Afrika ( AfDB), imetoa dola za Kimarekani Bilioni tisa tokea ilipoanza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1971.
Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Ayeodeji Adesina amesema hayo leo Juni 13, 2025 katika mahafali ya 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), ambapo chuo hicho kimemtunuku Shahada ya Heshima ya Sayansi.

Amesema, katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake kuanzia 2015 hadi 2025, jumla ya msaada wa kifedha kwa Tanzania umefika dola bilioni 4.73, sawa ba asilimia 53 ya mikopo yote ambayo benki hiyo imetoa kwa Tanzania katika kupindi chote cha miaka 54.
“Nimevutiwa sana na mwenendo wa uchumi wa Tanzania na uimara wake chini ya uongozi shupavu wa maono wa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake.
“Kwa msukumo wa ukuaji katika kilimo, utalii, huduma za kifedha, uzalishaji viwandani, ujenzi wa madini sambamba na sera thabiti za mwenendo wa uchumi wa fedha, ukuaji halisi wa pato la taifa la Tanzania ukiongezeka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023 hadi asilimia 5.6 mwaka 2024 ” amesema.
Amesema mwaka huu ukuaji huo unatarajiwa kuendelea hadi kufikia asilimua 5.9 na 6.0, na hivyo kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kasi kubwa zaidi ya ukuaji wa uchumi barani Afrka.

Amesema ndio maana benki hiyo imeongeza msaada wake kwa Tanzania katika kipindi cha miaka minne iliyopita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoka dola za Marekani Bilioni 2.25 kufikia Desemba 2021 hadi dola bilioni 3.74 kufikia Desemba 2024.
Dkt. Adesina amesema benki hiyo inaunga mkono mradi wa kishujaa wa Rais Samia uitwao ‘ Kujenga kesho iliyo bora’ kwa msaada wa dola milioni 130.
Vile vile benki hiyo ilitoa dola milioni 70 kwa ajili ya kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzanua ( TADB).
“Benki ya Maendeleo ya Afrika inaratibu jumla ya dola bilioni 3.2 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR), itakayounganisha Tanzania na Burundi pamoja na Hamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hivyo kuimarisha biashara na ujumuishaji wa kikanda, sambamba na kufungua fursa za madini,” amesema.
Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema katika Duru ya Kwanza ya Mahafali ya 55, chuo hicho kimehudhurisha wahitimu 829 wakiwemo wa shahada ya uzamivu, shahada ya umahiri, stashahada ya uzamili, shahada ya awali, stashahada na astashahada.
” Katika duru ya kwanza ya mahafali ya 55, wanawake katika shahada za awali ni asilimia 48, umahiri ni asilimia 49, na uzamivu ni asilimia 31 ya wahitimu wote,” amesema.
Amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kwa faida ya umma. Kwani elimu waliyoipata ni mali na faida ya jamii.
Pia amewataka wahitimu hao kuthibitisha uwezo wao kwa vitendo, kwani mabadiliko yanahitaji watu wanaothubutu.
“Sasa ni wakati wa kuchukua hatua, kuandika, kuzungumza kwa busara na kushughulikia changamoto za jamii kwa njia bunifu na yenye maadili.
Kwa upande wake Mkuu wa UDSM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema pamoja na hayo, Dkt. Adesina ni mdau mkubwa wa maendeleo hasa ya miundombinu.
“Huyu tuliyemtunuku benki yake ni mdau mkubwa kwa maendeleo,” amesema Kikwete.