Na Lucy Lyatuu
SERIKALI imeiagiza Taasisi Ya Teknolojia Dares Salaam (DIT) kuandaa taarifa itakayowezesha utekelezwaji wa utaratibu wa kupeleka wanafunzi nje ya nchi ili kujifunza na kupata ujuzi zaidi.
Waziri wa Elimu Sayansi Na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema hayo kwenye mahafali ya 19 duru ya kwanza ya DIT, Dar es Salaam ambapo wanafunzi wamehitimu kozi mbalimbali katika Taasisi hiyo.
Akizungumza, Mkenda amesema taarifa ya DIT inatakiwa ipeleke taarifa hiyo Wizarani ndani ya mwezi huu Desemba ambayo itasaidia serikali kujua bajeti inayotakiwa ili wanafunzi wanaosoma kozi mbalimbali katika Taasisi hiyo waweze kwenda kujifunza katika nchi nyingine na kupata ujuzi utakaowawezesha kuajirika na kujiajiri katika maeneo mbalimbali.

Amesema taarifa hiyo itawezesha Wizara kujua kwenye bajeti ya sasa inayoandaliwa iweze kupunguza matumizi ya maeneo mengine ili kutenga fedha kwa ajili ya kupeleka vijana chini ya mpango wa masomo kwa ushirikiano na taasisi za nje ujulikanao kama sandwich ili kuwawezesha vijana wa Tanzania kupata elimu na ujuzi zaidi.
Kadhalika amesema Serikali itazungumza na Ubalozi wa China ili kwamba ufadhili wa masomo wanaotoa kwa masomo katika vyuo vya nchini humo uwe chini ya mpango huo wa Sandwich hususani kwa wanaosomea kozi za uhandisi chuoni hapo.

Amesema DIT imeingia makubalino na Taasisi za Elimu China kwa ajili ya kupeleka wanafunzi kusoma katika vyuo hivyo yaani Sandwich program ambapo chini ya mpango huo mwanafunzi wa DIT anapelekwa nchini China kusoma kwa ngazi ya Diploma na anaporudi nchini anakamilisha taratibu za kupata shahada.
“Chini ya mpango wa Sandwich mwanafunzi wa DIT anapelekwa nchini China kusoma Diploma na anaporudi nchini anakamilisha taratibu za degree na kwamba mfumo huo unawezesha kuwa na ujuzi wa kufanya kazi katika kampuni mbalimbali za ndani na nje ya nchi,”amesema Mkenda.
Amesema wanafunzi wote wanaosomea uhandisi katika taasisi hiyo wapite katika mfumo huo wa sandwich ili vijana wapate ajira katika maeneo mbalimbali.
Aidha amesema katika kuboresha elimu nchini Wizara itatenga fedha chini ya utaratibu wa Samia Scholarship jambo litakalosaidia kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa elimu ujuzi ili vijana wapate ajira ndani na nje.

“Leteni taarifa kwenye bajeti ili mwanafumzi aende huko kunatakiwa nini ili fursa hizo ziwabebe wanafunzi hawa, ” Amesema.
Profesa Mkenda amewaambia wahitimu hao kuwa elimu haina mwisho, na wasijifungie ndani bali wajifunze kutoka kwa wengine nakuona kile wanachofanya ili waweze kufanya kazi kwa kwa ubora na kuongeza ujuzi zaidi.
Amesema katika utaratibu huo wa kupeleka wanafunzi nje ya nchi kujifunza wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kuanzia mwakani 2026 wataanza kupelekwa nje kujifunza zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya DIT, Dkt Richard Masika amewaambiwa wahitimu hao kuwa elimu bila matendo ni sawa na mti bila matunda na kwamba watumie ujuzi walioupata kitoa huduma yenye maudhui ya kitaalam.
Amewataka kujua kuwa ulimwengu unahitaji wabunifu na kuwasihi kuongeza bidii, nidhamu na ubunifu zaidi.
Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba amesema Katika kuhakikisha wanafunzi na waalimu wanapata fursa ya kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu na taasisi nyingine ndani na nje ya nchi taasisi ina makubaliano ya kushirikiana na taasisi zipatazo 50.

Amesema Makubaliano haya yana manufaa makubwa kwa Taasisi kwani wanafunzi wananufaika nayo.

