Na Lucy Lyatuu
DAWATI la Jinsia na Watoto la Polisi lililopo Madema, Unguja, likiungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Kwa
pamoja na Serikali ya Finland limetoa ulinzi na kuhakikisha usalama Kwa makundi ya watoto wa kike katika eneo hilo Kwa kuwaepusha na ukatili wa ndoa za utotoni.
Hatua hiyo imewezesha miongoni mwa watoto wa kike kutimiza ndoto zao,lakini pia wazazi wakiwezeshwa kushiriki mijadala elekezi iliyolenga kushughulikia mila na mitazamo inayochochea ndoa za utotoni.
Akitoa ushuhuda katika maadhimisho ya siku ya mwanamke, Zuhra (ambaye sio jina halisi) amesema elimu yake ilitarajiwa kukatishwa, utoto wake ungeisha ghafl kama ilivyo kwa wasichana wengi wanaokabiliwa na ndoa za utotoni.
Amesema alipokuwa na umri wa miaka 17 , mustakabali wake ulikuwa unaamuliwa na wengine.
“Sikuwa na uwezo mkubwa wa kupinga mpaka pale hatua moja muhimu ilipobadilisha kila kitu,” amesema na kuongea kuwa msaada huo haukumhusu Zuhra pekee bali na wazazi.
Amesema kupitia mchakato huo, familia ilifanya uamuzi mkubwa uliobadilisha maisha, ndoa iliyokuwa imepangwa ilifutwa, mahari ilirejeshwa, na wazazi wote wawili wakajitolea kuhakikisha watoto wao wote wanaendelea na masomo.
Amesema Baada ya kuondokana na tishio la ndoa ya utotoni, alirejea shuleni akiwa na ari mpya na Kwa sasa amemaliza elimu yake ya sekondari na anaendelea na masomo zaidi katika fani ya sheria.
Amesema ndoto yake ni kufanya kazi na wanawake na wasichana waliokumbwa na ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wengine wanaokabiliwa na hatari kama aliyowahi kukumbana nayo wanapatiwa ulinzi.
“Nataka kuwasaidia wasichana kuelewa haki zao na kujua kwamba ndoto zao zina thamani,” anasema.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, MarkSchreiner amesema Kuwezesha msichana kutimiza ndoto zake ni moja ya uwekezaji wenye nguvu zaidi wanaoweza kufanya.
“Kwa ushirikiano na wadau kama Serikali ya Finland, tunabadilisha ulinzi kuwa fursa na kuhakikisha hakuna msichana anayebaki nyuma.”amesema.
Amesema Siku ya Wanawake Duniani inakumbusha kwamba wasichana wanapopewa nafasi ya kudai haki zao na kufanya maamuzi yao wenyewe, jamii nzima inasogea karibu zaidi na usawa na haki.
Baba wa Zuhra, Zimbwe Msumi (jina limebadilishwa), anasema tukio hilo lilibadilisha kabisa uelewa wake kuhusu maana ya kumlinda binti yake.
Nawahimiza wazazi kote Tanzania kusimama kulinda haki za mtoto wa kike, kuwapeleka shule na kuwaunga mkono katika kutimiza ndoto zao. Tunapowalinda wasichana wetu, tunalinda mustakabali wetu.”

